NDOINYO AUNGA MKONO BAJETI ATAKA IWAWEZESHE WANANCHI WA VIJIJINI, TUJENGE UCHUMI WA KUJITEGEMEA, AOMBA BARABARA YA LAMI NGORONGORO

 NDOINYO: BAJETI IWAWEZESHE WANANCHI WA VIJIJINI, TUJENGE UCHUMI WA KUJITEGEMEA

Na Joseph Ngilisho, DODOMA 

Mbunge wa Ngorongoro, Yannick Ndoinyo, ameipongeza Serikali kwa kuwasilisha Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 akisema imejengwa katika misingi ya kukuza uchumi wa ndani, kuimarisha uwekezaji na kupanua wigo wa walipakodi, huku akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wananchi wa vijijini ambao ndio msingi wa uchumi wa taifa.

Akichangia mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali bungeni mjini Dodoma, Ndoinyo aliwapongeza viongozi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango kwa maandalizi ya bajeti hiyo, akieleza kuwa imeakisi maono na mwelekeo wa maendeleo unaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema bajeti hiyo ni ya kipekee kwa kuwa ndiyo ya kwanza kutekelezwa baada ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, jambo linaloifanya kuwa nyenzo muhimu ya kuweka msingi wa safari mpya ya maendeleo ya nchi kwa miongo ijayo.

Ndoinyo alisema moja ya mambo muhimu yaliyobebwa na bajeti hiyo ni jitihada za kuimarisha kundi la kati la wawekezaji na kurasimisha shughuli za sekta isiyo rasmi, hatua ambayo itaongeza idadi ya walipakodi na kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Tunapaswa kuwajengea uwezo wananchi wanaofanya shughuli katika sekta isiyo rasmi kwa sababu hawa ndio walipakodi wa kesho. Kadri tunavyowawezesha ndivyo tunavyopanua msingi wa mapato ya Serikali na kujenga uchumi imara zaidi,” alisema.

Hata hivyo, mbunge huyo alitaka Serikali kueleza kwa uwazi zaidi namna bajeti hiyo itakavyowanufaisha wananchi wa vijijini ambao ni zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania, akibainisha kuwa kundi hilo ndilo linalobeba shughuli kuu za uzalishaji nchini.

Alisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa unapaswa kuelekezwa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza tija, kipato cha wananchi na mchango wa sekta hizo katika pato la taifa.

“Ni muhimu kuona uwiano wa bajeti unaoonyesha wazi kiasi gani cha fedha kinaenda kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi ambao ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu,” alisema.

Ndoinyo pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa mamlaka za serikali za mitaa ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, akisema maendeleo ya wananchi yanategemea kwa kiasi kikubwa nguvu ya serikali za mitaa katika kusimamia huduma na miradi ya maendeleo.

Aidha, alisema bajeti hiyo imeonyesha hatua kubwa ya Tanzania kuelekea kujitegemea kifedha, baada ya sehemu kubwa ya matumizi ya Serikali kufadhiliwa na mapato ya ndani.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, uwezo wa kujitegemea unapaswa kuendelea kuongezwa ili kuondoa utegemezi wa misaada ya nje ambayo wakati mwingine huathiriwa na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ya nchi wahisani.

Katika mchango wake, Ndoinyo aliitaka Serikali kuongeza uwekezaji katika sekta ya mifugo, akieleza kuwa sekta hiyo bado haijapewa uzito unaostahili licha ya mchango wake mkubwa katika maisha ya wananchi wa maeneo mengi ya wafugaji nchini.

Pia alisisitiza umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Ngorongoro, hususan barabara ya lami inayounganisha maeneo ya Loliondo, akisema miundombinu hiyo ni muhimu katika kufungua fursa za kiuchumi na kuunganisha wananchi na masoko.

Alisema bila uwekezaji wa kutosha katika miundombinu, wananchi wa maeneo ya pembezoni wataendelea kushindwa kunufaika kikamilifu na fursa za maendeleo zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akihitimisha mchango wake, Ndoinyo alisema bajeti ya mwaka 2026/2027 imeonyesha dira sahihi ya maendeleo na ina uwezo wa kuimarisha uchumi wa wananchi endapo utekelezaji wake utaweka mkazo katika uzalishaji, uwezeshaji wa wananchi wa vijijini na maendeleo ya miundombinu.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم