MBUNGE WA EALA ATAKA MABADILIKO YA USIMAMIZI WA FEDHA NA KUHARAKISHWA KWA SARAFU MOJA YA AFRIKA MASHARIKI
Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
MBUNGE wa EALA, Kennedy Musyoka, ameitaka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kushughulikia changamoto zinazoweza kutatuliwa ndani ya taasisi zake kwa kuajiri watumishi wenye uwezo na sifa stahiki ili kuongeza ufanisi wa utendaji.
Akichangia mjadala wa ripoti ya bajeti, Musyoka alisema EAC haiwezi kuendelea kuendeshwa kwa kutegemea kanuni na taratibu za kifedha pekee, bali inahitaji sheria maalumu ya usimamizi wa fedha za umma na utawala wa kifedha ili kuimarisha uwajibikaji na kuondoa changamoto zinazojirudia.
Pia aliitaka Baraza la Mawaziri kutoa ufafanuzi kuhusu mfumo mpya wa uchangiaji wa fedha za Jumuiya, hususan kipengele kinachotaja “kukubalika” kwa fomula hiyo, akitaka kubainishwa ni nani anayepaswa kuidhinisha na muda gani utatumika ili kuepusha migongano katika mzunguko wa bajeti.
Aidha, mbunge huyo alisisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa sarafu moja ya Afrika Mashariki, akieleza kuwa licha ya kuongezeka kwa biashara ndani ya ukanda huo, wafanyabiashara bado wanakumbwa na gharama na usumbufu mkubwa wa kubadilisha fedha wanapofanya biashara kati ya nchi wanachama.
Musyoka alitoa mfano wa mfanyabiashara aliyeshindwa kupata Shilingi za Kenya katika benki moja jijini Dar es Salaam na kulazimika kupitia mchakato mrefu wa kubadilisha fedha, hali aliyosema inawaumiza wananchi wa Afrika Mashariki na kuathiri urahisi wa biashara za kikanda.
Mwisho, aliunga mkono ripoti hiyo huku akiitaka EAC kuchukua hatua za haraka katika masuala ya usimamizi wa fedha na utekelezaji wa ajenda ya sarafu moja.
Ends

Post a Comment