EAC YAPENDEKEZA BAJETI YA DOLA MILIONI 110.8 KWA MWAKA 2026/2027 ,TAASISI ZAJENGEWA UWEZO KWA DOLA MILIONI 70,
Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imewasilisha mapendekezo ya bajeti ya Dola za Marekani milioni 110.86 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikielekeza fedha hizo katika kuimarisha biashara ya kikanda, miundombinu, huduma za kijamii, usalama na kuendeleza agenda ya mtangamano wa kikanda.
Akiwasilisha bajeti hiyo mbele ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) mjini Arusha leo, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC, ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya EAC wa Uganda, Rebecca Alitwala Kadaga, alisema bajeti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia Mkakati wa Saba wa Maendeleo wa EAC (2026/27–2030/31) wenye lengo la kuimarisha ustawi wa wananchi wa Afrika Mashariki.
Kadaga alisema kati ya fedha hizo, Dola milioni 67.76 sawa na asilimia 62 zitachangiwa na nchi wanachama pamoja na mapato ya ndani ya jumuiya, huku Dola milioni 41.58 sawa na asilimia 38 zikitarajiwa kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Kwa mujibu wa mgawanyo wa bajeti hiyo, sekta ya kuimarisha uwezo wa taasisi za EAC, uwajibikaji na utoaji huduma imepewa sehemu kubwa zaidi ya Dola milioni 70.46. Aidha, Dola milioni 11.05 zimetengwa kwa ajili ya kukuza biashara ya ndani na nje ya ukanda, huku Dola milioni 10.67 zikielekezwa katika kuimarisha huduma za kijamii na mshikamano wa wananchi wa jumuiya hiyo.
Sekta ya uzalishaji na viwanda imepangiwa Dola milioni 7.2, wakati ushirikiano wa sera za fedha na utekelezaji wa Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki ukitengewa Dola milioni 4.12. Miundombinu ya kikanda imepangiwa Dola milioni 3.94 na masuala ya amani, usalama na utawala bora Dola milioni 3.42.
Katika mgawanyo wa fedha kwa taasisi za EAC, Sekretarieti ya EAC imepewa Dola milioni 59.76, ikifuatiwa na Bunge la Afrika Mashariki (EALA) lenye Dola milioni 19.16. Taasisi nyingine ni Baraza la Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) lenye Dola milioni 7.02, Chuo Kikuu cha Ushirikiano wa Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) Dola milioni 9.33 na Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) Dola milioni 5.01.
Kadaga alisema utekelezaji wa bajeti hiyo unatarajiwa kuongeza biashara ya ndani ya ukanda, kupunguza vikwazo visivyo vya ushuru, kuimarisha ushindani wa kiuchumi, kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya ukanda na kuharakisha utekelezaji wa Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki.
Alisema pia bajeti hiyo inalenga kuimarisha uthabiti wa mabadiliko ya tabianchi, kuboresha huduma za afya, elimu na ustawi wa jamii, pamoja na kupunguza gharama za biashara kwa kuboresha miundombinu ya usafiri na mawasiliano.
“Bajeti hii ni ahadi yetu kwa vijana kuwa mustakabali wao hauna mipaka, kwa wakulima kuwa soko lao ni la kikanda, na kwa kila mwananchi wa Afrika Mashariki kuwa ustawi wetu utagawanywa kwa usawa,” alisema Kadaga.
Bajeti hiyo sasa itajadiliwa na wabunge wa EALA kabla ya kupitishwa kwa ajili ya utekelezaji katika mwaka wa fedha unaoanza Julai 1, 2026.
Ends.



Post a Comment