MGOGORO WA EAC SI WA FEDHA, NI WA UONGOZI – GEORGE ODONGO

MGOGORO WA EAC SI WA FEDHA, NI WA UONGOZI – GEORGE ODONGO

Na Joseph Ngilisho|ARUSHA

 

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), George Odongo, amesema changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) si tatizo la kifedha kama ambavyo imekuwa ikielezwa mara kwa mara, bali ni mgogoro wa uongozi unaojitokeza kupitia matatizo ya fedha, rasilimali watu na utendaji wa taasisi za jumuiya hiyo.

Akichangia mjadala wa bajeti ya EAC,katika bunge la EALA linaloendelea jijini Arusha, Odongo alisema kwa miaka mingi wabunge wamekuwa wakijadili changamoto zilezile za ukosefu wa fedha, huku chanzo halisi kikiwa ni baadhi ya nchi wanachama kukosa dhamira na msimamo wa pamoja kuhusu ajenda ya ujumuishaji wa kikanda.

Alisema hata mabadiliko ya mfumo wa uchangiaji wa fedha unaozingatia uwezo wa uchumi wa kila nchi hayatakuwa suluhisho la kudumu ikiwa viongozi wa nchi wanachama hawataonyesha utashi wa kisiasa wa kutekeleza majukumu yao kwa jumuiya.

“Tunachokiita mgogoro wa kifedha ndani ya EAC ni matokeo ya mgogoro wa uongozi. Uongozi una matokeo, na tabia ya viongozi huathiri namna taasisi za nchi zinavyochukulia agenda ya ujumuishaji wa kikanda,” alisema.

Odongo alieleza kuwa baadhi ya nchi zimeendelea kutoa michango yao licha ya changamoto za kiuchumi, akitaja Burundi kama mfano wa nchi iliyoonyesha dhamira ya kuendeleza ushirikiano wa kikanda. Hata hivyo, alisema kuna baadhi ya nchi ambazo zimefikia hatua ya kutotoa mchango wowote kwa jumuiya kwa muda mrefu, jambo linaloibua maswali kuhusu kiwango cha kujitolea kwao.

Aidha, alionya kuwa bila kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa kikanda, EAC itaendelea kukabiliwa na changamoto za utekelezaji wa programu na malengo yake.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, ujumuishaji wa kikanda ni sehemu ya suluhisho la changamoto za uchumi na usalama zinazozikabili nchi za Afrika Mashariki, hivyo viongozi wa jumuiya wanapaswa kujenga kile alichokiita “mwingiliano wa mawazo na uelewa wa pamoja” ili kuimarisha mustakabali wa EAC.

Odongo alitoa wito kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za EAC kujadili kwa kina tofauti za kimtazamo zilizopo miongoni mwa nchi wanachama ili kuhakikisha jumuiya hiyo inasonga mbele kwa kasi na mwelekeo mmoja.

Ends

Post a Comment

أحدث أقدم