MELI TANO ZA IRAN ZAPITA HORMUZ KUFUATIA HATUA ZA AWALI ZA KUONDOA VIKWAZO
Na Arushadigital
Meli tano zimeripotiwa kufanikiwa kupita katika eneo lililokuwa chini ya udhibiti mkali wa Jeshi la Majini la Marekani katika Lango Bahari la Hormuz, kufuatia kuanza kutekelezwa kwa makubaliano yanayolenga kupunguza vikwazo vya usafiri wa baharini kati ya Marekani na Iran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, linalohusishwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC), meli hizo zinajumuisha meli tatu za kusafirisha mafuta ya Iran pamoja na meli mbili zilizobeba bidhaa muhimu kwa matumizi ya ndani.
Vyombo vya habari vya Iran vimeeleza hatua hiyo kuwa utekelezaji wa kwanza wa kivitendo wa makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni, yakilenga kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na nishati kupitia njia hiyo muhimu ya kimataifa.
Maendeleo hayo yanakuja wakati kukiwa na taarifa za kuwepo kwa makubaliano kati ya Marekani na Iran ya kufungua tena njia za usafiri katika Lango Bahari la Hormuz na kuanza kuondoa kwa awamu baadhi ya vizuizi vilivyowekwa kutokana na mvutano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili.
Hata hivyo, taarifa zinaonyesha kuwa baadhi ya washauri wa kijeshi wa Marekani wameonya kuwa hatua kadhaa za usalama bado zinaendelea kutekelezwa hadi pale makubaliano hayo yatakapokamilishwa na kurasimishwa kikamilifu.
Wakati huo huo, makampuni ya kimataifa ya usafirishaji wa meli yanaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo hayo, huku mengi yakisubiri uhakika zaidi wa usalama kabla ya kurejesha shughuli zake kwa kiwango cha kawaida katika eneo hilo.
Lango Bahari la Hormuz ni moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani, likipitisha sehemu kubwa ya mafuta na gesi inayosafirishwa kwa njia ya bahari, hivyo maendeleo yoyote katika eneo hilo yana athari kubwa kwa soko la nishati na uchumi wa dunia.

إرسال تعليق