MDOE AKARIBISHA WAWEKEZAJI KATIKA UTALII WA KANDA YA ZIWA

MDOE AKARIBISHA WAWEKEZAJI KATIKA UTALII WA KANDA YA ZIWA

Na Joseph Ngilisho | Arusha

Mtafiti kutoka Chuo cha Mipango, Dkt. Christopher Mdoe, amewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya utalii wa Kanda ya Ziwa, akisema eneo hilo lina vivutio vingi vya kipekee ambavyo bado havijatumika kikamilifu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi.

Dkt. Mdoe aliyasema hayo wakati wa Kongamano la Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Summit) linalofanyika jijini Arusha, ambapo aliwasilisha fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika utalii wa Kanda ya Ziwa Victoria kwa lengo la kuvutia mitaji na kuharakisha maendeleo ya sekta hiyo.

Alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuitangaza sekta ya utalii duniani kupitia vivutio maarufu vya Kanda ya Kaskazini, lakini bado kuna maeneo mengi yenye rasilimali za utalii ambazo hazijafahamika vya kutosha na wawekezaji pamoja na watalii.

“Kanda ya Ziwa ina hazina kubwa ya vivutio vya utalii. Tunawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika miundombinu ya utalii, huduma za malazi, usafiri wa majini na miradi mingine itakayosaidia kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” alisema.

Alisema juhudi hizo zinaunga mkono maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kusisitiza umuhimu wa sekta ya utalii katika kuongeza pato la taifa, kuvutia fedha za kigeni na kuimarisha ajira kwa Watanzania.

Dkt. Mdoe alifafanua kuwa Kanda ya Ziwa ina vivutio vingi vya asili, kihistoria na kitamaduni vinavyoweza kuwa bidhaa mpya za utalii nchini. Miongoni mwa vivutio hivyo ni visiwa vinavyopatikana ndani ya Ziwa Victoria, mandhari ya kuvutia ya asili, makazi ya ndege, hifadhi za wanyamapori pamoja na maeneo yenye historia ya tawala za machifu zilizokuwepo kabla ya uhuru.

Alitaja Kisiwa cha Ukerewe kuwa miongoni mwa maeneo yenye uwezo mkubwa wa kuvutia watalii kutokana na uwepo wa visiwa vidogo vingi vinavyounda mandhari ya kipekee. Aidha, Wilaya ya Muleba nayo ina visiwa na vivutio mbalimbali vinavyoweza kuendelezwa na kuwa sehemu muhimu ya utalii wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Dkt. Mdoe, tafiti zilizofanywa kwa ushirikiano kati ya watafiti na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) zimebaini kuwa Kanda ya Ziwa ina uwezo mkubwa wa kutoa uzoefu tofauti wa utalii ukilinganishwa na maeneo mengine ya nchi.

“Tunalenga kuendeleza utalii wa uzoefu ambapo mtalii atashiriki maisha halisi ya jamii zinazozunguka Ziwa Victoria. Ataweza kwenda kuvua samaki, kutega dagaa, kujifunza shughuli za uvuvi, kutembelea visiwa mbalimbali na kujionea utamaduni wa wenyeji,” alisema.

Aliongeza kuwa aina hiyo ya utalii itasaidia kuongeza muda wa watalii kukaa katika maeneo hayo, jambo litakaloongeza matumizi yao katika huduma za malazi, chakula, usafiri na bidhaa nyingine za ndani, hivyo kuwanufaisha wananchi wa maeneo husika.

Dkt. Mdoe alisema uwekezaji unaohitajika kwa sasa unahusisha ujenzi wa hoteli, vituo vya mapumziko, huduma za usafiri wa majini, miundombinu ya utalii pamoja na miradi mingine rafiki kwa mazingira chini ya mfumo wa Blue-Green Tourism.

“Hatutafuti kushindana na Serengeti, Ngorongoro au maeneo mengine maarufu ya utalii. Tunachotaka ni kuongeza chaguo kwa watalii wanaokuja Tanzania kwa kuwaandalia bidhaa mpya za utalii zinazokamilisha vivutio vilivyopo tayari,” alisema.

Aidha, aliwahamasisha wawekezaji kutembelea banda la UNDP katika kongamano hilo ili kujionea taarifa za kina kuhusu vivutio na fursa za uwekezaji zilizopo katika Kanda ya Ziwa.

Alisema uwekezaji katika sekta ya utalii wa Kanda ya Ziwa utasaidia kuongeza ajira, kukuza uchumi wa jamii zinazozunguka Ziwa Victoria na kuimarisha mchango wa sekta ya utalii katika maendeleo ya taifa.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post

Contact Form