WANANCHI ARUSHA WATOA USHUHUDA WA MAUMIVU MBELE YA TUME YA JAJI CHANDE
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
WANANCHI wa Jiji la Arusha wamejitokeza kwa wingi, bila kujali mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha, mbele ya Tume ya Uchunguzi ya Matukio ya Uvunjifu wa Amani inayoongozwa na Jaji mstaafu Mohammed Chande Othman, wakitoa ushuhuda wa masikitiko, maumivu na majonzi yaliyotokana na matukio ya vurugu wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kwa nyuso zilizojaa huzuni na sauti zenye uchungu, wananchi walieleza jinsi walivyopoteza ndugu zao kwa kupigwa risasi na askari wa polisi katika mazingira wanayodai hayakuwa ya haki.
Baadhi walisema marehemu walipigwa wakiwa wamesimama kwenye geti za nyumba zao, wengine walikuwa wakitoka sokoni kutafuta riziki, huku baadhi wakikumbwa na dhahama walizodai hawakuhusika nazo.
“Mwanangu hakushiriki maandamano yoyote. Alikuwa anatoka sokoni kununua chakula, akapigwa risasi mchana kweupe. Mpaka leo hatujui kosa lake lilikuwa nini,” alisema mwananchi mmoja huku akishindwa kuzuia machozi mbele ya wajumbe wa tume.
Mwananchi mwingine alisema ndugu yake alipigwa risasi akiwa amesimama getini nyumbani kwake. “Alikuwa anatazama kilichokuwa kinaendelea barabarani. Ghafla tukasikia risasi, akaanguka pale pale. Huyu mtu alikuwa raia asiye na hatia kabisa,” alieleza kwa masikitiko makubwa.
Katika kikao hicho, wananchi waliwasilisha malalamiko yanayohusu mauaji, vipigo, hofu, ghasia na ukosefu wa usalama, wakisisitiza kuwa matukio hayo yaliacha majeraha makubwa ya kisaikolojia na kijamii. Walitaka tume ichunguze kwa kina nani waliwajibika na kwa nini nguvu ya silaha ilitumika dhidi ya raia wasiojihami.
Akizungumza katika kikao hicho, Jaji Chande alisema tume imeundwa kwa lengo la kusikiliza kwa uwazi kilio cha wananchi na kubaini ukweli wa yaliyojiri. “Hii ni fursa ya wananchi kusema ukweli wao.
Tunalenga kuchunguza kila taarifa kwa kina na kutoa mapendekezo yatakayozingatia haki, ukweli na uwazi,” alisema.
Wananchi walisisitiza umuhimu wa uwazi katika mchakato mzima wa uchunguzi, wakisema wanahitaji majibu ya kina kuhusu sababu zilizopelekea vurugu hizo, matumizi ya risasi kwa raia, na hatua za kisheria zitakazochukuliwa ili kuzuia matukio kama hayo yasijirudie tena.
“Tume isiishie kusikiliza tu, tunahitaji haki. Waliopoteza maisha warudishiwe heshima yao na waliohusika wawajibishwe,” alisema mwananchi mwingine kwa sauti ya majonzi, akishangiliwa na waliokuwepo ukumbini.
Wajumbe wa tume walitilia mkazo umuhimu wa ushirikiano wa wananchi, wakibainisha kuwa ushahidi wa pande zote unahitajika ili kuhakikisha uchunguzi unakuwa wa haki, wa kweli na wenye lengo la kuimarisha amani ya kudumu.
Hadi sasa, Tume ya Jaji Chande inaendelea kukusanya ushahidi kutoka kata na maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza bila woga ili kila sauti isikike.
Tume inatarajiwa kuhitimisha uchunguzi wake na kutoa ripoti ya mwisho ambayo itawekwa wazi kwa umma, ikiwa na mapendekezo yanayolenga kurejesha imani ya wananchi, kuimarisha usalama na kuzuia marudio ya matukio ya uvunjifu wa amani nchini.
Ends..

0 Comments