MORANI 400 WAVAMIA MAKANISA MONDULI ,WATEKA WACHUNGAJI,WAWAVUA NGUO NA VIATU NA KUWATESA KWA KIPIGO WAWATEMBEZA UCHI PORINI KWA MASAA SITA WAKIWACHAPA FIMBO,MWENYEKITI WA KIJIJI NAYE AWINDWA!

Morani 400 wadaiwa kuvamia makanisa Monduli, wachungaji wanne watekwe na kuteswa

Na Joseph Ngilisho – MONDULI


KUNDI la morani wa Kimasai zaidi ya 400 wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha, wanadaiwa kuvamia makanisa mawili katika kijiji cha Lepurko na kuwateka wachungaji wanne, kisha kuwatesa kwa kuwapiga fimbo na kuwatembeza umbali mrefu porini wakiwa hawana viatu wala nguo, wakishinikiza waoneshwe binti aliyekuwa ameozeshwa na baba yake na baadaye kutoroka.







Picha za Mateso ya Nyanguro kwa wachungaji

Tukio hilo linadaiwa kutokea Januari 4, 2026, wakati wa ibada ya Jumapili, ambapo morani hao waliingia makanisani hadi madhabahuni na kuwashusha wachungaji waliokuwa wakiongoza ibada, wakiwatuhumu kuwapotosha watoto wa kike dhidi ya mila na desturi za Kimasai kutokana na imani za dini zinazokinzana na tamaduni za jamii hiyo.

Wachungaji wanaodaiwa kuteswa wakiwa chini ya ulinzi wa Morani

Miongoni mwa waliotekwa ni Mchungaji Amani Melau wa Kanisa la EAGT, Isaya Kanari (Kanisa la Baptisti), Lazaro Kanari (Katibu wa Kanisa la Baptisti) na Eliya Seuri. Wanne hao walidai kuvuliwa nguo na viatu, kisha kutembezwa porini kwa takribani saa sita kuanzia saa sita mchana hadi saa kumi na mbili jioni huku wakichapwa fimbo.

“Walikuja vijana wengi wakiwa wamebeba marungu na fimbo, wakaingia hadi madhabahuni, wakatutoa kwa nguvu na kutupeleka porini. Walikuwa wakituuliza kwa nini tunajitenga na mila za Kimasai na wakitutaka tuwaoneshe binti aliyekimbia ndoa,” alisema Mch. Melau.

Aliongeza kuwa lengo kubwa la mateso hayo lilikuwa kuwashinikiza wachungaji hao kufichua alipo binti aliyekuwa ameozeshwa na baba yake mara baada ya kuhitimu elimu ya kidato cha nne, lakini alitoroka kwa madai ya kutoridhishwa na ndoa hiyo. Binti huyo (jina limehifadhiwa) alidaiwa kuwa muumini wa moja ya makanisa hayo.

Kwa upande wake, Mchungaji Isaya Kanari alisema alikamatwa kwa nguvu wakati akiendesha ibada licha ya Mwenyekiti wa Kijiji kuwazuia vijana hao. “Mwenyekiti alijaribu kuwaomba wasifanye vurugu wala kunichukua, lakini walikataa na kuniweka mikononi mwao,” alisema.

Katibu wa Kanisa la Baptisti, Lazaro Kanari, alisema alijeruhiwa vibaya miguu baada ya kutembezwa porini kwenye miiba na mawe huku akipigwa fimbo, hali iliyomsababishia maumivu makali na kushindwa kutembea vizuri.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kijiji cha Lepurko, Samweli Melembuki, alisema naye ni mwathirika wa tukio hilo, akidai vitisho na mashambulizi yalielekezwa pia kwake kutokana na imani yake ya Kikristo. Alisema vijana hao walimkuta kanisani siku ya tukio, kisha siku iliyofuata walimfuata nyumbani kwa lengo la kumpiga wakimuhoji kwa nini anaabudu kanisani na kujitenga na mila za Kimasai.

“Waliniambia wazi kuwa suala hilo lina msukumo kutoka kwa viongozi wakuu wa kimila (Laigwanani), hivyo mimi kama mwenyekiti siwezi kuingilia kati. Walidai kwa kushindwa kwangu kuzuia tukio la kuwatesa wachungaji, hata mimi nijitayarishe kujitetea,” alisema Melembuki.

Aliongeza kuwa siku ya Jumatatu alinusurika kipigo baada ya vijana hao kufika nyumbani kwake, akieleza kuwa tukio hilo linaashiria kuhusika kwa baadhi ya wazee wa mila, jambo analodai linahatarisha amani na mshikamano wa kijiji.

Baada ya tukio hilo, waathirika walisema wametoa taarifa polisi kwa ajili ya uchunguzi na kuchukuliwa kwa hatua za kisheria, wakitaka kulindwa kwa usalama wao, kuheshimiwa kwa uhuru wa kuabudu na kudhibiti vitendo vya kikatili vinavyokiuka haki za binadamu na utawala wa sheria.

Ends..


Post a Comment

0 Comments