By Arushadigital-DAR ES SALAAM
Raia wawili wa China, Weisi Wang (41) na Yao Licong (32), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kukabiliwa na mashitaka mawili mazito, likiwemo kuongoza genge la uhalifu na utakatishaji wa fedha, yanayodaiwa kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Washitakiwa hao walisomewa mashtaka yao leo, Januari 7, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Mawakili wa Serikali waandamizi Patrick Mwita, Benjamin Muroto na Rhoda Mwakamela.
Akiwasilisha hoja za mashtaka, Wakili Benjamin Muroto alidai kuwa katika shitaka la kwanza, Wang na Licong wanadaiwa kuwa kati ya Desemba 1, 2024 hadi Desemba 30, 2025, katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza na Unguja – Zanzibar, pamoja na maeneo mengine nchini, walipanga na kuendesha genge la uhalifu lililojihusisha na kughushi nyaraka, kutengeneza kadi za benki feki, na kutoa fedha kwenye mashine za ATM kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kukwepa kodi.
Katika shitaka la pili la utakatishaji fedha, upande wa mashtaka unadai kuwa washitakiwa hao, kwa nyakati na maeneo hayo hayo, walipata mali isiyokuwa halali ikiwemo dola za Marekani 707,075 na shilingi milioni 281.71, huku wakijua au kuwa na sababu ya kuamini kuwa fedha hizo zilitokana na uhalifu wa kuendesha genge la kihalifu.
Upande wa Jamhuri uliieleza Mahakama kuwa uchunguzi wa kesi bado unaendelea, hivyo ukaomba washitakiwa waendelee kushikiliwa mahabusu hadi pale upelelezi utakapokamilika. Mahakama ilikubaliana na ombi hilo.
Kutokana na asili ya mashtaka hayo, Mahakama iliwatahadharisha washitakiwa kutotoa majibu yoyote kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 21, mwaka huu, itakaporudi kwa ajili ya kutajwa tena.
Ends


0 Comments