MTORO WA GEREZA ALIYEKUWA AKITUMIKIA KIFUNGO CHA MIAKA 30 AKAMATWA, AHUSISHWA NA MATUKIO YA UJAMBAZI NA UBAKAJI MBEYA
Na Arushadigital | MBEYA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia kijana aliyefahamika kwa jina la Siwema Yona Simfukwe (24), anayidaiwa kutoroka gerezani Mei 13, 2026 alipokuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi, baada ya kutoroka gerezani mtuhumiwa huyo alihusishwa na matukio mbalimbali ya uhalifu wa kutumia nguvu yaliyotokea katika eneo la Iwambi, jijini Mbeya, yakiwemo ya uvunjaji wa nyumba, uporaji na ubakaji.
Polisi wameeleza kuwa Mei 15, 2026, mtuhumiwa huyo alivamia nyumba moja akiwa na panga na kutishia kumuua mtoto aliyekuwapo ndani ya nyumba hiyo. Baada ya hapo, aliwafunga kwa kamba wakazi wa nyumba hiyo kabla ya kuwabaka mama wa familia pamoja na mfanyakazi wa ndani.
Katika tukio hilo, mtuhumiwa huyo anadaiwa kupora simu mbili za mkononi aina ya iPhone pamoja na fedha taslimu kiasi cha Shilingi 400,000.
Aidha, uchunguzi wa polisi unaonesha kuwa Mei 22, 2026, mtuhumiwa huyo alihusika katika tukio jingine la uporaji ambapo alimnyang’anya mwananchi simu aina ya iPhone 11 na kumlazimisha kutoa nywila ya simu hiyo. Baada ya kupata nywila hiyo, alidaiwa kuhamisha Shilingi 300,000 kutoka kwenye akaunti ya fedha ya mhanga.
Kutokana na mfululizo wa matukio hayo, Jeshi la Polisi kupitia kikosi maalum cha kupambana na uhalifu lilianzisha msako mkali uliodumu kwa siku kadhaa na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo Mei 30, 2026 majira ya saa 10:30 jioni katika eneo la Chipaka, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe.
Wakati wa kukamatwa kwake, polisi walimkuta akiwa na silaha ya kienyeji, panga, risasi moja ya shotgun pamoja na mizura miwili.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mara baada ya kukamatwa, baadhi ya wananchi waliokuwa eneo hilo walijaribu kumshambulia mtuhumiwa huyo kwa hasira kutokana na tuhuma zinazomkabili. Hata hivyo, askari polisi waliingilia kati na kufanikiwa kumuokoa kabla ya kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili ya matibabu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za wahalifu na watuhumiwa wa vitendo vya uhalifu, huku likisisitiza kuwa litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vinavyokiuka sheria za nchi.
Polisi wameeleza kuwa uchunguzi wa matukio hayo unaendelea huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa dhidi ya mtuhumiwa mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote za uchunguzi na matibabu.

Post a Comment