MBUNGE EALA APENDEKEZA NCHI ZINAZOKWEPA MICHANGO ZISIMAMISHWE UANACHAMA

MBUNGE EALA APENDEKEZA NCHI ZINAZOKWEPA MICHANGO ZISIMAMISHWE UANACHAMA

Na Joseph Ngilisho, ARUSHA

Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA),Kim Rut Gai amesema kuna haja ya kuchukuliwa hatua kali dhidi ya nchi wanachama zinazoshindwa kutekeleza wajibu wao wa kuchangia fedha za uendeshaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Akichangia mjadala bungeni katika Makao Makuu ya EAC jijini Arusha, mbunge huyo alisema baadhi ya nchi zimekuwa zikichelewesha au kutolipa michango yao kwa miezi mingi jambo linaloathiri utekelezaji wa shughuli na mipango ya jumuiya.

Alisema kuna wakati taasisi za EAC zimeendelea kufanya kazi kwa miezi minane hadi tisa bila kupokea fedha zinazotakiwa kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama, hali inayoweka shinikizo kubwa katika uendeshaji wa shughuli za jumuiya.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, suluhisho la kudumu ni kwa serikali za nchi husika kutekeleza kikamilifu masharti ya Mkataba wa EAC yanayohusu ulipaji wa michango na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya nchi zinazokaidi wajibu huo.

“Tunapaswa kutekeleza mkataba wetu. Nchi ambazo hazilipi michango yao zinapaswa kuwekewa vikwazo, ikiwemo kusimamishwa baadhi ya haki za uanachama hadi zitakapotekeleza wajibu wao,” alisema.

Aliongeza kuwa hatua hizo zitasaidia kuimarisha uwajibikaji miongoni mwa nchi wanachama na kuhakikisha kuwa programu na miradi ya maendeleo ya EAC haikwamishwi kutokana na ukosefu wa fedha.

Kauli hiyo imekuja wakati EALA ikiendelea kujadili masuala mbalimbali ya kifedha na utendaji wa taasisi za jumuiya kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na maendeleo ya kikanda.

Post a Comment

أحدث أقدم