SERIKALI KUJENGA BARABARA YA LAMI KWENDA HOSPITALI YA OLRUMETI ARUMERU
Na Joseph Ngilisho-Arushadigital| DODOMA
SERIKALI imesema itaanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya kilomita mbili kwa kiwango cha lami inayoelekea Hospitali ya Wilaya ya Olrumeti, Wilaya ya Arumeru, baada ya mradi huo kuingizwa katika bajeti na mipango ya maendeleo ya sekta ya barabara.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Juni 22 ,2026 na Naibu Waziri anayesimamia sekta ya barabara alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dk. Johannes Lukumay, ambaye alitaka kufahamu ni lini Serikali itatekeleza agizo la Waziri Mkuu la kujenga kipande hicho muhimu cha barabara.
Akiwasilisha swali lake, Dk. Lukumay alisema Februari 22, 2026 Waziri Mkuu alifanya ziara katika Jimbo la Arumeru Magharibi na kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Olrumeti, ambako alijionea uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya.
Mbunge huyo alisema pamoja na uwekezaji huo mkubwa, hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya barabara, hususan kipande cha kilomita mbili kinachounganisha hospitali na mtandao mkuu wa barabara, jambo linaloathiri usafiri wa wagonjwa, watumishi wa afya na wananchi wanaofika kupata huduma.
“Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa TARURA kuhakikisha barabara hiyo inajengwa na hata alieleza kuwa hakukuwa na ulazima wa kuomba kibali kingine. Sasa Serikali itatekeleza lini maelekezo hayo?” alihoji Dk. Lukumay.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri alisema Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo kwa kuwa inahudumia hospitali ya wilaya inayotoa huduma kwa maelfu ya wananchi wa Arumeru na maeneo jirani.
Alisema tayari maelekezo ya Waziri Mkuu yamefanyiwa kazi kwa kuingiza mradi huo katika bajeti za Serikali na kwamba taratibu za kibajeti na utekelezaji zinaendelea ili kuhakikisha ujenzi unaanza haraka iwezekanavyo.
“Tunatambua kwamba haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tayari tumeyaingiza katika mipango yetu na tuko katika hatua za utekelezaji. Lengo ni kuhakikisha kipande hicho cha barabara kinajengwa kwa kiwango cha lami ili kuboresha huduma za usafiri na afya katika eneo hilo,” alisema.
Hatua hiyo inatarajiwa kuondoa adha ya usafiri kwa wananchi wa Arumeru Magharibi na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Olrumeti, ambayo imeendelea kuwa kituo muhimu cha huduma za matibabu katika wilaya hiyo.
Ends..


إرسال تعليق