ALLY MEKU AWATAKA WANACCM KUJITENGA NA MAANDAMANO YA JULAI 7, ATOA TAHADHARI YA VURUG
Na Joseph Ngilisho| Arusha
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Arusha, Ally Mwinyimvua maarufu kwa jina la Ally Meku, amewasihi wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitenga na maandamano yanayodaiwa kuitishwa kupitia mitandao ya kijamii tarehe Julai 7, 2026, akieleza kuwa usalama wa wananchi unapaswa kupewa kipaumbele kuliko jambo lolote.
Meku alitoa wito huo alipokuwa mgeni rasmi katika kikao cha kutoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha miezi sita kilichoandaliwa na Diwani wa Kata ya Osunyai, Elirehema Nnko, kwa wajumbe na viongozi mbalimbali wa CCM wa kata hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Meku alisema kuwa historia inaonyesha kuwa maandamano na vurugu za kisiasa zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa wananchi wasio na hatia, hivyo ni muhimu kwa wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuwa waangalifu na kuepuka kushiriki matukio ambayo yanaweza kuhatarisha maisha yao.
Alisema bado ana kumbukumbu ya matukio ya vurugu yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, ambapo watu wengi walipoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa katika mazingira ya sintofahamu.
"Tuna wajibu wa kulinda amani na usalama wa nchi yetu. Mimi binafsi bado nina kumbukumbu ya matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi ambapo wananchi wengi walipata madhara makubwa. Miongoni mwa walioathirika walikuwa raia wa kawaida ambao hawakuwa sehemu ya migogoro yoyote," alisema Meku.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kujifunza kutokana na matukio yaliyopita na kuepuka kushiriki maandamano au mikusanyiko inayoweza kusababisha machafuko, hasa pale ambapo mazingira ya usalama hayajathibitika.
Meku aliwataka wanachama wa CCM katika Kata ya Osunyai na maeneo mengine kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo kwa amani badala ya kujihusisha na maandamano yanayoweza kuleta taharuki katika jamii.
"Ninawasihi wana CCM kukaa majumbani na kuendelea na shughuli zao za kila siku. Tusikubali kushawishiwa kuingia kwenye mazingira ambayo yanaweza kuhatarisha maisha yetu na ya familia zetu. Amani ndiyo msingi wa maendeleo yetu," alisisitiza.
Aidha, aliwataka viongozi wa chama katika ngazi mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na utulivu wa nchi, akieleza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana katika mazingira ya migogoro na vurugu.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Osunyai, Elirehema Nnko, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kipindi cha miezi sita iliyopita, akieleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali za maendeleo ndani ya kata hiyo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa CCM wa kata, wajumbe wa jumuiya mbalimbali za chama pamoja na wananchi waliofika kufuatilia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Kata ya Osunyai.
Ends..





إرسال تعليق