SERIKALI KUJENGA “COLD ROOMS” KUPUNGUZA UPOTEVU WA MAZAO ARUMERU MAGHARIBI
Na Arushadigital, DODOMA
Serikali imesema iko tayari kusaidia ujenzi wa vituo vya kisasa vya kuhifadhi mazao (cold rooms) katika maeneo yanayojihusisha na kilimo cha mboga mboga, ikiwemo Jimbo la Arumeru Magharibi mkoani Arusha, ili kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna.
Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri husika wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ambaye alitaka kujua mpango wa serikali kusaidia wakulima wa maeneo ya Bangata na Kata ya Elkidinga wanaopoteza mazao yao mara baada ya kuvuna.
Katika swali lake, Dkt. Lukumay alieleza kuwa wakulima wa mboga mboga katika jimbo hilo wanakabiliwa na changamoto ya uhifadhi wa mazao, hali inayosababisha hasara kubwa licha ya uzalishaji kuwa mzuri.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri alisema serikali tayari ina mpango wa kitaifa wa kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno (post-harvest losses), ambapo ujenzi wa maghala ya kisasa ya baridi ni sehemu ya mkakati huo.
“Mheshimiwa Spika, nimthibitishie Mheshimiwa Dkt. Johannes kwamba niko tayari kuongozana naye kutembelea jimbo lake mara baada ya Bunge la Bajeti. Aidha, serikali ina mpango wa kujenga cold rooms katika maeneo yote yanayolima mboga mboga ili kupunguza upotevu wa mazao,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya ziara hiyo, serikali itafanya tathmini na kuchukua hatua stahiki kulingana na mahitaji halisi ya wakulima wa eneo husika.
Hatua hiyo inatarajiwa kuwa mkombozi kwa wakulima wa Arumeru Magharibi na maeneo mengine nchini, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa masoko ya uhakika na miundombinu ya kuhifadhi mazao yao.
Ends..

0 Comments