LUKUMAY AIBUA CHANGAMOTO YA VIWANJA ARUMERU MAGHARIBI, AOMBA UWEKEZAJI WA MICHEZO
By Arushadigital|DODOMA
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ameibua changamoto ya upungufu wa miundombinu ya viwanja vya michezo katika jimbo lake, akitaka hatua za haraka kuchukuliwa ili kuimarisha sekta hiyo na kunufaisha vijana.
Dkt. Lukumay alitoa ombi hilo alipokutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Christian Paul Makonda, ambapo alimweleza kuwa ukosefu wa viwanja bora vya michezo umekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya vipaji vya vijana katika eneo hilo.
Katika maelezo yake, mbunge huyo aliomba serikali kuona uwezekano wa kujenga kiwanja cha kisasa cha michezo katika Jimbo la Arumeru Magharibi, akieleza kuwa uwekezaji huo utachochea maendeleo ya michezo na kutoa fursa kwa wananchi kunufaika na mashindano makubwa ya kimataifa, ikiwemo AFCON.
“Ujenzi wa kiwanja cha michezo utatoa fursa kwa vijana wetu kuendeleza vipaji vyao na pia kuwezesha jimbo letu kushiriki kikamilifu katika matukio makubwa ya michezo barani Afrika,” alisisitiza.
Aidha, Dkt. Lukumay alitumia fursa hiyo kumwomba nyota wa soka wa kimataifa kutoka Ivory Coast, Didier Drogba, kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika jimbo hilo kwa kuanzisha akademi ya michezo (Sports Academy). Alieleza kuwa uwepo wa akademi hiyo utakuwa chachu ya kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana katika michezo mbalimbali.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya serikali na wadau wa kimataifa katika sekta ya michezo unaweza kuleta mapinduzi makubwa kwa vijana wa Tanzania, hususan wale wa Arumeru Magharibi, kwa kuwapa jukwaa la kuonyesha na kukuza vipaji vyao.
Kwa upande wake, Waziri Makonda aliahidi kulichukua suala hilo kwa uzito na kulifanyia kazi, akisisitiza dhamira ya serikali katika kukuza sekta ya michezo nchini kama sehemu ya ajenda ya maendeleo ya vijana.
Hatua hiyo inaonekana kuwa ni sehemu ya jitihada za viongozi kuimarisha sekta ya michezo nchini, sambamba na kukuza ajira na vipato kwa vijana kupitia vipaji vyao.

0 Comments