KIKONGWE (90) ADAIWA KUBAKWA, AVUNJIWA MKONO MOSHI; IMANI ZA KISHIRIKINA ZAHUSISHWA
Na Joseph Ngilisho, MOSHI
Kikongwe mwenye umri wa miaka 90, mkazi wa kijiji cha Maua Kibosho, Kata ya Kibosho Kati, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kubakwa kikatili na mtu aliyejulikana kwa jina la Justin Masawe, tukio lililosababisha kuvunjika kwa mkono wake wakati akitekeleza unyama huo, tukio lililoacha mshangao na hofu kwa jamii.
Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa Aprili 23, 2026 nyumbani kwa muathirika, huku baadhi ya wananchi wakilihusisha na imani potofu za kishirikina, wakihisi huenda mhalifu alifanya kitendo hicho kwa nia ya kujipatia utajiri WA mali.
Kwa mujibu wa familia ya muathirika, kikongwe huyo alikutwa katika hali mbaya asubuhi iliyofuata, akilalamika maumivu makali mwilini na sehemu za siri na kushindwa kutumia mikono yake baada ya kuvunjika.
Mmoja wa ndugu wa karibu, Lidia James Masawe, alisema alimkuta kikongwe huyo akiwa hawezi hata kushika kikombe cha chai kutokana na maumivu makali.
“Aliniambia kuna mtu alikuja usiku, akamshika kwa nguvu akawa hawezi kupumua, akamlalia mikono hadi ikavunjika. Pia alieleza kuwa alifanyiwa ukatili wa kingono na kuumizwa sana,” alisema Lidia kwa masikitiko.
Familia hiyo imeeleza kuwa kabla ya tukio hilo, kikongwe huyo alikuwa na hali yake ya kawaida japo Huwa hasikii Wala kuona kutokana na umri wake, lakini sasa hali yake imezorota zaidi na wakati mwingine hupoteza fahamu.
Kutokana na tukio hilo, ndugu na majirani waliamua kuimarisha ulinzi kwa kupanga doria za usiku, hatua iliyosaidia kufanikisha kukamatwa kwa kijana mmoja anayehusishwa na tukio hilo.
Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limethibitisha kumshikilia mtuhumiwa huyo kwa mahojiano zaidi, huku likiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Wananchi wa eneo hilo wameeleza kushtushwa na tukio hilo, wakilitaja kuwa ni la kinyama na lisilokubalika, huku wakitoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika.
Aidha, wito umetolewa kwa jamii kuachana na imani potofu za kishirikina ambazo zinaweza kuchochea vitendo vya ukatili, hususan dhidi ya wazee.
NB: Picha kwa hisani ya Mtandao haihusiani na tukio hili.
Ends.


0 Comments