PROF. NDUNGURU ATOA KAULI NZITO BAADA YA KUTUNUKIWA TUZO YA MFANYAKAZI HODARI NA RAIS SAMIA
Na Joseph Ngilisho|ARUSHA
MKURUGENZI wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru, amesema tuzo aliyotunukiwa ni chachu ya kuongeza kasi ya mageuzi na utendaji bora ndani ya taasisi hiyo, akiahidi kuifanya kuwa kinara barani Afrika katika udhibiti wa afya ya mimea.
Prof. Ndunguru alitoa kauli hiyo ofisini kwake Mei 5 ,2026 jijini Arusha, wakati akizungumza na vyombo vya habari, kufuatia kutunukiwa tuzo ya Mfanyakazi Hodari na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua mchango wake katika kuongoza mageuzi makubwa ya kiutendaji yaliyoifanya TPHPA kuongeza mapato kwa kasi na kuwa taasisi ya mfano.
Tuzo hiyo ilitolewa juzi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa mkoani Njombe, ambapo Rais aliwatambua watumishi waliobobea kwa ubunifu, uadilifu na matokeo chanya kwa Taifa.
Akizungumza kwa msisitizo, Prof. Ndunguru alisema mafanikio hayo si ya mtu mmoja bali ni matokeo ya ushirikiano wa wafanyakazi wa mamlaka hiyo pamoja na wadau wa sekta ya kilimo.
“Kwa kweli hii tuzo naipokea kwa niaba ya timu nzima ya TPHPA. Imetupa nguvu mpya ya kuendelea kufanya mageuzi zaidi, kuongeza ufanisi na kuhakikisha tunalinda uzalishaji wa mazao nchini,” alisema.
Alieleza kuwa katika kipindi kifupi, mamlaka hiyo imefanikiwa kuimarisha udhibiti wa visumbufu vya mimea ikiwemo wadudu na magonjwa, hatua iliyochangia kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula na kufikia utoshelevu wa zaidi ya asilimia 130.
Aidha, alisema maboresho ya mifumo ya ukusanyaji mapato pamoja na uwekezaji katika miundombinu, hasa katika ofisi za mipakani, yamechangia ongezeko kubwa la mapato ya serikali ndani ya miaka mitatu iliyopita.
Prof. Ndunguru pia alibainisha kuwa mamlaka hiyo imeanza kutumia teknolojia za kisasa ikiwemo droni katika kudhibiti milipuko ya wadudu waharibifu kama viwavi jeshi na ndege waharibifu aina ya kwelea kwelea, hatua iliyosaidia kupunguza hasara kwa wakulima.
“Kwasasa tuna droni zaidi ya 20 na tunaendelea kuongeza nyingine ili kuimarisha operesheni zetu za kudhibiti visumbufu vya mimea kwa haraka na ufanisi,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuimarisha sekta ya kilimo kupitia sera na uwekezaji unaolenga kuongeza uzalishaji na kukuza mauzo ya mazao nje ya nchi.
Alisema TPHPA ina mipango ya kupanua huduma zake kwa kusogeza ofisi karibu na wakulima, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya kikanda katika maeneo ya uzalishaji wa mazao ya kimkakati kama parachichi, viazi na mbogamboga.
“Dira yetu ni kuona TPHPA inakuwa mamlaka ya mfano barani Afrika katika udhibiti wa afya ya mimea. Tuzo hii ni mwanzo wa safari mpya ya mafanikio makubwa zaidi,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Prof. Ndunguru, mafanikio ya taasisi hiyo yanakwenda sambamba na malengo ya taifa ya kukuza uchumi na kuongeza kipato cha wananchi kupitia sekta ya kilimo.
Alitoa wito kwa wafanyakazi na wadau kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaendelezwa na kuimarishwa zaidi kwa manufaa ya taifa.
Katika hatua nyingine Profesa Ndunguru aliwakaribisha wadau wote wa Afya ya Mimea kushiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Afya ya Mimea, ambayo hufikia kilele chake tarehe 12 mwezi huu jijini Dodoma, ikiwa ni Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea. Hii ni fursa muhimu ya kukutana, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za kuimarisha sekta ya kilimo.
Ends..





0 Comments