LATRA YAANZA KUNG'ATA ARUSHA, YAKAMATA DALADALA 45 KWA KUTOZA NAURI KUBWA YATISHIA KUZIFUTA BARABARANI

 Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Kanda ya Arusha imeanza operesheni maalum ya kukabiliana na wamiliki na madereva wa daladala wanaokiuka viwango vya nauli vilivyowekwa na serikali, ambapo zaidi ya magari 45 tayari yamekamatwa na kutozwa faini kali.

Hatua hiyo imekuja sambamba na onyo kali la kufungiwa leseni kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri watakaoendelea kukaidi maelekezo ya serikali.

Utekelezaji wa nauli mpya za daladala jijini Arusha ulianza rasmi Mei Mosi mwaka huu, ukiwa na lengo la kudhibiti ongezeko holela la nauli na kulinda maslahi ya abiria.

Akizungumza na waandishi wa habari,ofisni kwake Mei 5,2026 Afisa Usafirishaji, Omari Ayubu, alisema kuwa viwango hivyo vipya vimepangwa kwa kuzingatia umbali wa safari ili kuhakikisha haki na usawa kwa watumiaji wa usafiri wa umma.

Alieleza kuwa safari zisizozidi kilomita 10 zitatozwa Sh700, huku safari za hadi kilomita 15 zikitozwa Sh800.
“Katika jiji la Arusha, safari nyingi zinaangukia katika viwango hivi, hivyo wananchi wengi watanufaika na mfumo huu mpya wa nauli,” alisema Ayubu.

Alitoa mfano kuwa abiria wanaosafiri kutoka maeneo ya Chekereni au Moshi hadi stendi ndogo—umbali wa takribani kilomita saba—wanapaswa kulipa Sh700, huku wanaovuka maeneo kama Relini kuelekea katikati ya jiji wakitarajiwa kulipa Sh800 kulingana na umbali.

Kwa mujibu wa Ayubu, serikali pia imeelekeza mabasi yote ya daladala kubandika jedwali maalum la nauli (fare chart) ndani ya magari ili kuongeza uwazi na kupunguza migogoro kati ya abiria na wahudumu.

“Hatua hii itasaidia kila abiria kufahamu kiwango halisi cha nauli na hivyo kupunguza ubishani usio wa lazima,” alisisitiza.

Hata hivyo, licha ya kuanza kwa utekelezaji huo, baadhi ya madereva na makondakta wameendelea kupuuza viwango hivyo, hali iliyosababisha kuanzishwa kwa ukaguzi mkali barabarani.

Ayubu alisema ndani ya wiki moja tu, zaidi ya magari 45 yamekamatwa kwa kosa la kutoza nauli zaidi ya kiwango kilichowekwa.

“Kutoza nauli zaidi ya iliyoelekezwa ni kosa la kisheria. Hatutasita kuchukua hatua kali, ikiwemo kusimamisha huduma kwa wahusika,” alionya.

Aidha, aliwataka abiria kudai haki zao wanapolipa nauli, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanapewa chenji sahihi.

“Ni dhuluma kumnyima abiria chenji yake. Wananchi wasisite kudai haki zao,” alisisitiza.

Katika kuimarisha usimamizi, serikali imewahimiza wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu madereva na makondakta wanaokiuka taratibu, kupitia namba maalum zilizotolewa.

Wakati huo huo, baadhi ya viongozi wa serikali wakiwemo wakuu wa wilaya wameanza kushuka barabarani kusimamia utekelezaji wa viwango hivyo, hatua inayolenga kuhakikisha sheria zinafuatwa kikamilifu.

Ayubu alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na wananchi ili kufanikisha mfumo huo mpya wa nauli.

Akiongea malalamiko kuhusu nauri usafiri wa Bajaji alifafanua kuwa vyombo vya usafiri wa kukodisha kama bajaji, bodaboda na teksi, hutumia mfumo wa makubaliano kati ya dereva na abiria katika kupanga nauli.

Hali hiyo inamaanisha kuwa nauli za bajaji zinaweza kutofautiana kulingana na maelewano ya pande mbili.

“Mfano, leo dereva anaweza kutoza Sh500 na kesho Sh2,000, kulingana na makubaliano. Hii ni kwa sababu bajaji ni usafiri wa kukodisha,” Alisema

Kutokana na changamoto ya usafiri , mamlaka imeanza kupanua huduma za daladala katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakitegemea zaidi bajaji, ili kuwapa wananchi chaguo la usafiri wenye nauli elekezi na nafuu.

Wananchi wametakiwa kuelewa kuwa wanapochagua kutumia bajaji, wanakuwa wamekubaliana na masharti ya nauli kwa hiari yao, tofauti na daladala ambazo zinafuata viwango rasmi vilivyowekwa na serikali.

Mamlaka imewataka wananchi katika maeneo ambayo bado hayana huduma ya daladala kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe haraka kuboresha upatikanaji wa usafiri wa uhakika na wa gharama nafuu.

Ends .

Post a Comment

0 Comments