RAIS SAMIA AMPATIA TUZO PROFESA NDUNGURU, AITANGAZA TPHPA KUPAA KIUTENDAJI NA MAPATO

 RAIS SAMIA AMPATIA TUZO PROFESA NDUNGURU, AITANGAZA TPHPA KUPAA KIUTENDAJI NA MAPATO

Na Arushadigital|NJOMBE 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtunuku tuzo ya Mfanyakazi Hodari Mkurugenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru, kufuatia mageuzi makubwa ya kiutendaji yaliyoiwezesha taasisi hiyo kuongeza mapato kwa kasi na kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.

Tuzo hiyo ilitolewa juzi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa, ambapo Rais Samia aliwatambua wafanyakazi waliobobea katika utumishi wa umma kwa ubunifu, uadilifu na matokeo chanya kwa Taifa.



Profesa Ndunguru, ambaye anatoka Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Taasisi za Utafiti (RAAWU), alijiunga na TPHPA mwaka 2023. Tangu wakati huo, ameiongoza taasisi hiyo katika mabadiliko makubwa ya kimfumo, kiufundi na kiutawala yaliyoongeza ufanisi na tija.

Chini ya uongozi wake, TPHPA imefanikiwa kuboresha na kuimarisha maabara zake na kuzifanya za kisasa, pamoja na kuziunganisha katika mfumo mmoja wa kidijitali unaosomana katika ofisi 47 zilizopo mipakani mwa Tanzania. Mfumo huo umeongeza kasi ya upimaji wa viuatilifu na kudhibiti uingizaji wake nchini.

Matokeo ya mageuzi hayo ni ongezeko kubwa la mapato ya taasisi hiyo kutoka shilingi bilioni 14 mwaka 2023 hadi kufikia bilioni 69 ndani ya miezi minane tu kuanzia Julai 2025 hadi Februari 2026—hatua inayotajwa kuwa ya kihistoria katika sekta hiyo.

Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Samia aliwapongeza wafanyakazi wote nchini kwa mchango wao katika kukuza uchumi na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha maslahi yao.

“Chapeni kazi kwa bidii. Serikali inatambua mchango wenu, na kadri hali ya uchumi inavyoimarika, tutaendelea kuboresha maslahi yenu, kulipa madeni ya wafanyakazi na kutafuta fursa zaidi za ajira zenye staha ndani na nje ya nchi,” alisema Rais Samia.

Kwa upande wake, Profesa Ndunguru alisema ushindi huo ni matokeo ya ushirikiano madhubuti kati ya Serikali na wafanyakazi wa TPHPA, pamoja na utekelezaji wa maelekezo ya Rais kwa vitendo.

“Huu si ushindi wangu binafsi, bali ni wa timu nzima ya TPHPA. Ndani ya miaka mitatu, tumepiga hatua kubwa kiasi cha kuvutia watafiti na wanasayansi kutoka nchi mbalimbali za Afrika kuja kujifunza kutoka kwetu,” alisema.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yameondoa utegemezi wa maabara za nje ya nchi kwa wafanyabiashara wa mazao ya kilimo, kwani sasa vipimo vya ubora vinafanyika ndani ya Tanzania katika maabara zilizoidhinishwa kimataifa.

“Zamani tulipeleka mazao yetu kupimwa nje ya nchi kabla ya kuyauza kimataifa. Leo hii tunajitegemea—maabara zetu zinatambulika kimataifa na zinatoa ithibati inayokubalika,” alisisitiza.

Aidha, alisema TPHPA imeongeza mchango wake kwa wakulima kwa kuwasaidia kuzalisha mazao salama na yenye ubora, sambamba na kuwatafutia masoko ya kimataifa. Alibainisha kuwa kampuni 16 zinazojihusisha na mazao ya parachichi na viazi mviringo tayari zimepatiwa fursa ya masoko nchini China.

Katika kuimarisha zaidi sekta hiyo, Profesa Ndunguru alisema ujenzi wa maabara mpya unaendelea katika makao makuu ya TPHPA Arusha, huku nyingine ikitarajiwa kujengwa Makambako ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakulima na wafanyabiashara.

Vilevile, alifichua mpango wa kujenga benki ya mbegu za asili yenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya mbegu 10,000, hatua inayolenga kulinda urithi wa kilimo na kuimarisha tafiti za kisayansi.

Kwa sasa, taasisi hiyo ina uwezo wa kuchambua sampuli zaidi ya 2,000 kwa wiki, jambo lililopunguza kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa utoaji wa ithibati.

Katika hatua nyingine, Profesa Ndunguru aliahidi kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari (JOWUTA) kuwajengea uwezo wanahabari ili kusaidia kuelimisha umma na kufichua biashara haramu ya viuatilifu visivyoidhinishwa.

Naye Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma, alimpongeza Profesa Ndunguru pamoja na wafanyakazi wa TPHPA kwa kazi kubwa wanayofanya, huku akiishukuru mamlaka hiyo kwa kuwa miongoni mwa wadhamini wa tuzo za wanahabari hodari mwaka 2026.



MWISHO

Post a Comment

0 Comments