MBUNGE LUKUMAY HAPOI, ACHUKUA HATUA ZA HARAKA KUTATUA KERO YA BARABARA NGARAMTONI–SELIANI, AGREDA LAWASILI ENEO LA TUKIO

 MBUNGE LUKUMAY ACHUKUA HATUA ZA HARAKA KUTATUA KERO YA BARABARA NGARAMTONI–SELIANI, AGREDA LAWASILI ENEO LA TUKIO

Na Joseph Ngilisho| ARUMERU

MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ameendelea kuonesha dhamira ya dhati katika kushughulikia changamoto za miundombinu zinazoikabili jamii yake, baada ya kuchukua hatua za haraka kufuatia uharibifu mkubwa wa barabara inayounganisha Ngaramtoni na Hospitali ya Seliani.

Tukio hilo lilijiri jana, Mei 2, 2026, wakati mbunge huyo akiwa safarini kuelekea Kata ya Mwandet, alipokutana na kundi la vijana wafanyabiashara wa eneo la Ngaramtoni waliomueleza kwa uchungu hali mbaya ya barabara hiyo iliyoharibiwa vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha.

Kwa mujibu wa vijana hao, uharibifu huo umekuwa kikwazo kikubwa kwa shughuli zao za kila siku, hususan usafirishaji wa bidhaa na upatikanaji wa huduma muhimu za afya katika Hospitali ya Seliani, hali inayowaweka katika mazingira magumu kiuchumi na kijamii.

Akizungumza papo hapo, Dkt. Lukumay aliwahakikishia wananchi hao kuwa Serikali tayari imeshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo, na kwamba kazi kamili ya ujenzi itaendelea mara tu mvua zitakapopungua.

Hata hivyo, akionesha utayari wa kutatua changamoto hiyo bila kusubiri, mbunge huyo aliwasiliana mara moja na viongozi wa TANROADS, akisisitiza umuhimu wa kupitisha greda kwa ajili ya kuchonga barabara hiyo ili iweze kupitika kwa muda wakati mkandarasi akisubiri kuanza rasmi ujenzi baada ya hali ya hewa kutengemaa.

Hatua hiyo imeanza kuzaa matunda kwa kasi, ambapo leo Mei 3, 2026, greda limewasili katika eneo hilo na kuanza kazi ya marekebisho, hatua inayolenga kurejesha mawasiliano muhimu kati ya Ngaramtoni na Hospitali ya Seliani.

Wananchi wa eneo hilo wamepongeza juhudi hizo, wakieleza kuwa ni ushahidi wa uongozi unaosikiliza na kuchukua hatua kwa wakati. Wamesema ujio wa greda ni faraja kubwa kwao na unarejesha matumaini ya kuendelea na shughuli zao bila vikwazo vikubwa.


Kwa upande wake, Mbunge Lukumay ameendelea kusisitiza kuwa atahakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati, akilenga kuboresha maisha ya wananchi wa Arumeru Magharibi.

Hatua hiyo pia imeibua pongezi kwa Serikali kwa ujumla, huku wananchi wakieleza kuwa ni “Serikali sikivu inayojali mahitaji ya wananchi wake,” hasa katika nyakati ngumu kama hizi za mvua zinazosababisha changamoto za miundombinu.

Kwa sasa, macho na masikio ya wananchi wa Ngaramtoni na maeneo jirani yameelekezwa katika utekelezaji wa ahadi ya ujenzi kamili wa barabara hiyo, wakiamini kuwa juhudi zinazoendelea ni mwanzo wa suluhisho la kudumu.

Ends..

Post a Comment

0 Comments