DKT LUKUMAY ATEMBELEA UBOVU WA BARABARA MWANDETI ATOA KAULI NZITO KUHUSU BARABARA NA MADARAJA HATARISHI ARUMERU MAGHARIBI, APIGA SIMU ,SERIKALI YAMHAKIKISHIA MATENGENEZO

 LUKUMAY ATOA KAULI NZITO KUHUSU BARABARA NA MADARAJA HATARISHI ARUMERU MAGHARIBI, WANANCHI WALIA MATESO

Na Joseph Ngilisho | ARUMERU

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ametoa kauli nzito na kuahidi hatua za haraka kufuatia kilio cha wananchi wa Kata ya Mwandeti kuhusu hali mbaya ya barabara na madaraja yaliyoharibiwa na mvua za mafuriko.

Kauli hiyo imekuja baada ya wananchi wa vijiji vya Engutoto, Losikito, Embibiya na Engalaon kueleza kwa uchungu changamoto kubwa ya miundombinu, ikiwemo barabara kuu inayounganisha maeneo hayo ambayo imeharibika vibaya na kuwa ngumu kupitika, huku madaraja mawili muhimu yakiwa katika hatari ya kusombwa na maji.


Akizungumza mbele ya wananchi, Dkt. Lukumay alisema haikubaliki kwa wananchi kuendelea kuishi katika mazingira hatarishi kutokana na miundombinu duni, akibainisha kuwa madaraja yaliyopo katika barabara hiyo yameathiriwa vibaya na mmomonyoko wa udongo uliosababishwa na mafuriko.

“Madaraja yaliyopo hatarini ni pamoja na daraja la kitongoji cha Shuleni katika kijiji cha Engutoto pamoja na daraja la Loibanguti lililopo Losikito. Miundombinu hii ni muhimu kwa mawasiliano na shughuli za wananchi wetu, hivyo hatuwezi kuiacha katika hali hii,” alisema Lukumay.

Aliongeza kuwa sehemu kubwa ya udongo unaoyazunguka madaraja hayo imechukuliwa na maji na kusababisha makorongo makubwa, hali inayoongeza uwezekano wa madaraja hayo kusombwa wakati wowote mvua zitakapoendelea kunyesha.

“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan haitaki kuona wananchi wake wanapata mateso ya namna hii. Nimepokea kilio chenu na ninaenda kukifanyia kazi mara moja. Hatutakubali vijiji hivi vikatikwe mawasiliano,” alisisitiza.

Mbunge huyo alieleza kuwa tayari ameanza mawasiliano na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ili kuhakikisha hatua za dharura zinachukuliwa kuimarisha barabara na madaraja hayo kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Alisema kipaumbele cha kwanza ni kuokoa madaraja hayo mawili, akionya kuwa yakisombwa, wananchi watakosa huduma muhimu kama afya, elimu na biashara, hali itakayodhoofisha uchumi wa eneo hilo.

Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Engutoto, kitongoji cha Shuleni, walieleza masikitiko yao wakisema daraja hilo limekuwa chanzo cha ajali za mara kwa mara, majeraha na hata vifo, huku likikarabatiwa mara kwa mara bila kujengwa kwa ubora wa kudumu.

“Mara nyingi wanakuja kulikarabati lakini halijengwi kwa ubora. Hapa watu wanaanguka na wengine kupoteza maisha. Hata mzazi wangu alianguka hapa na kufariki dunia,” alisema mmoja wa wananchi kwa huzuni.

Wananchi hao walieleza kuwa daraja hilo ni kiungo muhimu kinachowaunganisha na shule, hospitali na huduma nyingine za kijamii, hivyo kuharibika kwake kunasababisha usumbufu mkubwa, hasa wakati wa mvua ambapo magari hushindwa kupita na wanafunzi kukosa masomo.

Sauti ya kilio hicho iliungwa mkono na mkazi wa Losikito, Boniface Samweli, ambaye alimlilia mbunge huyo akisema hali ya barabara katika eneo hilo imekuwa mbaya kiasi cha kuhatarisha maisha ya wakazi, hususan watoto wa shule, wagonjwa na wajawazito.

“Mheshimiwa Mbunge, hali ya barabara ni mbaya sana. Watu hawawezi kupita kwa urahisi, hata watoto wa shule wanaogopa kupita asubuhi kutokana na hatari iliyopo njiani,” alisema Samweli.

Aliongeza kuwa barabara inayoingia Losikito pamoja na ile inayounganisha Likamba kuelekea soko la Kisongo imechakaa vibaya, hali inayowafanya wananchi kushindwa kusafirisha mazao na kufikia huduma muhimu kwa wakati.

Kwa mujibu wa Samweli, baadhi ya maeneo kama Rulutume yameathirika zaidi, ambapo umbali mfupi wa takribani kilomita mbili hulazimika kuzungukwa hadi kufikia kilomita 11 kutokana na ubovu wa barabara.

“Kunapokuwa na dharura, hasa kwa mama mjamzito, ni vigumu kabisa kupita. Wakati mwingine inalazimu kuzunguka umbali mrefu sana, jambo linaloweka maisha yao hatarini,” alisisitiza.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wameiomba Serikali kuingilia kati kwa haraka kwa kujenga madaraja imara na kuboresha barabara kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya eneo hilo.

Akihitimisha, Dkt. Lukumay aliwataka viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha wanakusanya taarifa sahihi za uharibifu wa miundombinu na kuziwasilisha kwa wakati, huku akiahidi kufuatilia suala hilo hadi ngazi za juu ili liingizwe katika mipango ya bajeti kwa ajili ya suluhisho la kudumu.

Aliwataka wananchi kuwa na subira wakati hatua za dharura zikichukuliwa, akisisitiza kuwa Serikali haitowaacha wapambane peke yao katika changamoto hiyo inayotishia maisha na maendeleo ya wananchi wa Kata ya Mwandeti.
















Ends

Post a Comment

0 Comments