MBUNGE ARUMERU MAGHARIBI AIBUA CHANGAMOTO YA USAFIRI KWA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII, AMUALIKA WAZIRI KUFANYA ZIARA
Na Joseph Ngilisho|ARUSHADIGITAL
MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ameeleza bungeni changamoto kubwa ya usafiri inayokabili Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, akisisitiza kuwa hali hiyo inakwamisha utoaji wa huduma kwa wananchi hususan katika maeneo ya vijijini yenye mazingira magumu kufikika.
Akizungumza wakati wa kikao husika cha bunge, Dkt. Lukumay alimweleza Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Onesphoro Gwajima, kuwa maafisa maendeleo ya jamii wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa vitendea kazi muhimu ikiwemo magari na pikipiki, hali inayopunguza ufanisi wao katika kuwafikia wananchi na kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Mbunge huyo alifafanua kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha ina jiografia yenye changamoto, ikiwemo maeneo ya milimani na vijiji vilivyotawanyika kwa umbali mkubwa, jambo linalohitaji uwekezaji wa kutosha katika sekta ya usafiri ili kuhakikisha huduma za maendeleo ya jamii zinawafikia wananchi wote kwa usawa.
Alibainisha kuwa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo hayatoshi kugharamia ununuzi wa magari na pikipiki kwa ajili ya divisheni za maendeleo ya jamii, hivyo kuomba Serikali Kuu kuingilia kati kwa kuweka utaratibu maalum wa kuziwezesha idara hizo kwa vitendea kazi vinavyohitajika.
“Ni muhimu Serikali ikaangalia namna ya kuziwezesha divisheni hizi kwa usafiri, kwani zinahusika moja kwa moja na makundi nyeti ya jamii wakiwemo wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum,” alisisitiza Dkt. Lukumay.
Katika hatua nyingine, Mbunge huyo alitumia fursa hiyo kumwalika Waziri Gwajima kufanya ziara ya kikazi katika Jimbo la Arumeru Magharibi, ili aweze kujionea hali halisi na kuzungumza moja kwa moja na wananchi.
Alieleza kuwa ziara hiyo itatoa nafasi kwa Waziri kukutana na wanawake, vijana na makundi maalum, kusikiliza changamoto zao na kuweka mikakati ya kuzitatua kwa vitendo.
“Tunamkaribisha Mheshimiwa Waziri aje Arumeru Magharibi ili apate nafasi ya kuonana na wananchi na kusikiliza kero zao moja kwa moja, jambo litakalosaidia kuboresha huduma na sera zinazogusa maisha yao,” aliongeza.
Ombi hilo linaakisi jitihada za wabunge kuishauri Serikali kuimarisha sekta ya maendeleo ya jamii, ambayo ina mchango mkubwa katika ustawi wa makundi mbalimbali na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Ends..


0 Comments