TARSI YAJITOSA MAPAMBANO YA AJALI BARABARANI ,YATOA MAFUNZO KWA WADAU WA USALAMA BARABARANI

 TARSI YAJITOSA MAPAMBANO YA AJALI BARABARANI ,YATOA MAFUNZO KWA WADAU WA USALAMA BARABARANI 

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

TAASISI ya Mpango wa Usalama Barabarani Tanzania (TARSI) imesema itaendelea kuongoza juhudi za kupunguza ajali za barabarani nchini kwa kuwekeza zaidi katika elimu ya usalama, uboreshaji wa usanifu wa miundombinu na ushirikiano wa karibu kati ya wadau wote wa sekta ya usafiri.

 

Akizungumza katika mafunzo ya siku tano ya kitaalamu ya wadau wa usalama barabarani yaliyofunguliwa jijini Arusha na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Riziki Shemdoe, Mkurugenzi Mtendaji wa TARSI, Marick Barongo, alisema mapambano dhidi ya ajali hayawezi kufanikiwa bila elimu kuanzia ngazi ya usanifu hadi kwa watumiaji wa mwisho wa barabara.

Barongo alisema elimu ya usalama barabarani ndiyo silaha ya msingi katika kupunguza vifo vinavyotokana na ajali, akisisitiza kuwa changamoto nyingi huanzia kwenye hatua za awali za ujenzi wa barabara.

“Usalama barabarani hauanzi barabarani, unaanzia kwenye meza ya usanifu. Kama wahandisi watazingatia viwango vya usalama, tunapunguza kwa kiasi kikubwa hatari zote zinazoweza kuzuilika,” alisema Barongo.

Alibainisha kuwa hadi sasa TARSI imewafikia zaidi ya wahandisi 800 waliopatiwa mafunzo maalum ya kuzingatia usalama katika miradi ya barabara, hatua inayolenga kuhakikisha miundombinu inakuwa rafiki kwa watumiaji wote.

Aidha, alisema taasisi hiyo pia imeweka programu za kuwafikia madereva kwa kushirikiana na kampuni za usafirishaji pamoja na kampeni za elimu kwa watembea kwa miguu, ili kujenga tabia salama katika matumizi ya barabara.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Hospitali ya Mifupa Moi, Dr. Joel , alisema ajali za barabarani bado ni chanzo kikuu cha wagonjwa katika vitengo vya dharura nchini.

Alisema hospitali hupokea takribani wagonjwa 8,000 kwa mwaka, ambapo zaidi ya nusu hutokana na ajali, wengi wao wakiwa na majeraha makubwa ya kichwa, mgongo na mifupa.

“Chanzo kikubwa ni tabia za watumiaji wa barabara—ulevi, mwendo kasi na kutofuata sheria,” alisema.

Aliongeza kuwa kampeni ya “Vaa Helmet, Ubongo Hauna Spare” inalenga kupunguza majeraha kwa waendesha pikipiki, ambao wameendelea kuwa kundi linaloongoza kwa ajali.

Mwenyekiti wa Bodi ya TARSI, Vicent Minja, alisema suluhisho la ajali linahitaji ushirikiano wa serikali, sekta binafsi na jamii, kuanzia hatua ya kupanga na kubuni barabara.

Alisema miundombinu mingi bado haizingatii usalama wa watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na bodaboda, hali inayochangia ongezeko la ajali.

“Tunahitaji kuhakikisha kila barabara inazingatia usalama tangu hatua ya usanifu,” alisema.

Alibainisha pia kuwa taasisi kama TANROADS, TARURA na Road Fund Board (Tanzania) zimehusishwa ili kupata suluhisho la pamoja.

Meneja wa Usalama na Usanifu wa Barabara nchini kutoka Norplan Tanzania Limited, Laurent Maganga, alisema elimu ya usalama barabarani inapaswa kuingizwa rasmi kwenye mitaala ya uhandisi ili kuhakikisha wataalamu wanajenga miundombinu salama na yenye kuzingatia maisha ya watu.

Alisema ajali zinaendelea kuigharimu nchi kwa kupoteza maisha, ulemavu na gharama kubwa za matibabu, hali inayohitaji hatua za haraka.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Riziki Shemdoe alisema kuwa Taasisi ya TARSI imekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya uhandisi nchini tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002, ambapo tayari imeshatoa mafunzo kwa wahandisi zaidi ya 800.

Waziri Shemdoe amesema mafunzo hayo ni chachu muhimu katika jitihada za kupunguza ajali za barabarani nchini, akisisitiza kuwa ni lazima mafunzo hayo yaendelee kuimarishwa na kupanuliwa ili kuongeza ufanisi wa wataalamu wa uhandisi.

Aidha, ameitaka TARURA kuhakikisha inaandaa na kuratibu mafunzo ya mara kwa mara kwa wahandisi wake, ili kuwezesha ujenzi na ukarabati wa barabara unaozingatia viwango na alama za kimataifa, hatua ambayo itaongeza ubora wa miundombinu na kupunguza hatari za ajali barabarani.

Ends..

Post a Comment

0 Comments