MVUTANO WAZIDI KUCHACHAMA HORMUZ: MELI ZA INDIA ZASHAMBULIWA, BIASHARA YA MAFUTA DUNIANI YATIKISIKA

 MVUTANO WAZIDI KUCHACHAMA HORMUZ: MELI ZA INDIA ZASHAMBULIWA, BIASHARA YA MAFUTA DUNIANI YATIKISIKA

By Arushadigital 

Mvutano wa kijeshi katika Ghuba ya Uajemi umeingia hatua mpya baada ya meli mbili za India kushambuliwa na Jeshi la Iran zilipokuwa zikijaribu kuvuka katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, saa chache baada ya Tehran kutangaza kurejesha vizuizi katika njia hiyo nyeti ya kimataifa ya usafirishaji wa mafuta.

Kwa mujibu wa vyanzo vya India, meli hizo zililengwa kwa risasi za onyo kutoka vikosi vya majini vya Iran, hali iliyozilazimu baadhi yao kusitisha safari na kurejea nyuma ili kuepuka madhara zaidi. Tukio hilo linaashiria kuongezeka kwa msimamo mkali wa Iran katika kudhibiti njia hiyo muhimu ya kimkakati.

Hatua ya Iran inatajwa kuhusishwa moja kwa moja na mvutano wake unaoendelea na Marekani, huku mamlaka za Tehran zikisisitiza kuwa hazitaruhusu meli zozote kupita katika eneo hilo hadi pale masuala ya kiusalama yatakapopatiwa ufumbuzi. Ripoti zinaeleza kuwa baadhi ya meli zilipokea maonyo makali kupitia mawasiliano ya redio zikizuiwa kuingia katika eneo hilo, huku nyingine zikilazimika kubadili mwelekeo kutokana na hofu ya kushambuliwa.

Mlango wa Bahari wa Hormuz unabaki kuwa mhimili mkuu wa usafirishaji wa nishati duniani, ukipitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa kimataifa. Kufungwa au kudhibitiwa kwa njia hiyo kuna athari za moja kwa moja kwa uchumi wa dunia, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa bei za mafuta, kuathirika kwa minyororo ya usambazaji, na kuongeza taharuki katika masoko ya kimataifa.

Wakati hali ikiendelea kuwa tete, juhudi za kidiplomasia zinaendelea kimya kimya kujaribu kupunguza mvutano huo. Hata hivyo, wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaonya kuwa endapo suluhu ya haraka haitapatikana, mgogoro huo unaweza kuongezeka na kusababisha athari kubwa zaidi katika usalama wa kikanda na uchumi wa dunia.

#Ar

Post a Comment

0 Comments