BABA AHUKUMIWA MIAKA 30 JELA KWA KOSA LA KUZINI NA MAHARIMU MKINGA
Na Arushadigital-TANGA
Mahakama ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Aprili 15, 2026, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, mkazi wa Kijiji cha Kigongoi, Tarafa ya Maramba, Kilimo Katua Isaya (30), baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kuzini na maharimu dhidi ya binti yake wa kumzaa.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, ukiwemo ushahidi wa kitaalamu wa vipimo vya vinasaba (DNA), uliothibitisha bila shaka kuwa mtoto aliyezaliwa ni wa mshtakiwa mwenyewe.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa mahakamani, mshtakiwa alifanya kitendo hicho kinyume cha maumbile na sheria za nchi, hali iliyosababisha binti huyo kupata ujauzito na baadaye kujifungua mtoto. Tukio hilo lilielezwa kuwa la kikatili na linalokiuka kwa kiwango kikubwa maadili ya jamii pamoja na haki za mtoto.
Akizungumza wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Benedict Matunduka, aliieleza Mahakama kuwa ushahidi uliopo unaonesha wazi hatia ya mshtakiwa, na kuomba adhabu kali itakayokuwa fundisho si tu kwa mtuhumiwa bali pia kwa jamii nzima.
“Adhabu hii iwe onyo kwa watu wengine wenye mienendo kama hii, hasa katika kipindi ambacho vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukiukwaji wa haki za watoto vinaonekana kuongezeka,” alisema Matunduka.
Mahakama, katika uamuzi wake, ilisisitiza kuwa haitakuwa na muhali kwa watu wanaojihusisha na makosa ya aina hiyo, na kwamba itaendelea kutoa adhabu kali ili kulinda usalama wa watoto, utu wa binadamu pamoja na maadili ya jamii kwa ujumla.
Aidha, Mahakama imewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa mapema wanapobaini viashiria vya vitendo vya ukatili wa kijinsia, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa wakati na kuzuia madhara zaidi.
Hukumu hiyo imekuja wakati juhudi mbalimbali zikiendelea nchini kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kulinda haki za watoto, ambapo wadau wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa elimu kwa jamii pamoja na utekelezaji madhubuti wa sheria.

0 Comments