ASKARI POLISI AUAWA KWA KUPIGWA NA KUNDI LA WANANCHI ARUSHA, WATU SITA WASHIKILIWA
Na Joseph Ngilisho| Arusha
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya askari polisi, Roland Mollel, mkazi wa Arusha, aliyefariki dunia baada ya kushambuliwa usiku wa Aprili 15, 2026 katika mazingira yanayodaiwa kuchangiwa na taharuki ya wananchi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo, tukio hilo la kusikitisha lilitokea katika mtaa wa Mlimani, kata ya Muriet, jijini Arusha, ambapo kundi la wananchi lilichukua hatua za mkono wa sheria baada ya kusambaa kwa taarifa zisizothibitishwa kuhusu uwepo wa wezi katika eneo hilo.
Kamanda Masejo alieleza kuwa marehemu, ambaye ni askari polisi, alikuwa amemaliza majukumu yake ya kikazi na alikuwa akiendelea na shughuli zake binafsi wakati tukio hilo linatokea. Inadaiwa kuwa wakati huo alikuwa amepanda pikipiki akiwa ameongozana na mtu mwingine anayedhaniwa kuwa dereva bodaboda.
“Katika hali ya sintofahamu iliyotokana na uvumi wa kuwepo kwa wezi, kundi la watu lilianza kuwashambulia wawili hao bila kuwahoji au kuthibitisha ukweli wa taarifa hizo, na kusababisha shambulio lililopelekea kifo cha askari huyo,” alifafanua Kamanda Masejo.
Amesema baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita wanaodaiwa kuhusika moja kwa moja na tukio hilo, huku msako mkali ukiendelea kuwatafuta wengine wanaosadikiwa kushiriki katika mauaji hayo.
Aidha, Kamanda Masejo alisisitiza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo pamoja na kuwabaini washiriki wote, ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mkononi, likionya kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na vinaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwemo kuua au kujeruhi watu wasio na hatia.
“Wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama badala ya kuchukua hatua kwa mihemko, kwani kufanya hivyo kunahatarisha maisha ya watu na kuvuruga utaratibu wa kisheria,” alisisitiza.
Tukio hilo limeibua huzuni na masikitiko miongoni mwa wakazi wa Arusha, huku likiibua upya mjadala kuhusu madhara ya uvumi na hatua za haraka zisizo na uthibitisho katika jamii.

0 Comments