BODI YA SEKONDARI KORONA YAMTAKA Paul Makonda KUWA MLEZI, YAPENDEKEZA SHULE IBEBE JINA LAKE
Na Joseph Ngilisho| ARUSHA
Bodi ya Shule ya Sekondari Korona iliyopo jijini Arusha, imeibuka na pendekezo zito la kumtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kuwa mlezi wa shule hiyo huku ikienda mbali zaidi kwa kupendekeza shule hiyo ibadilishwe jina na kupewa jina la kiongozi huyo.
Pendekezo hilo lililotangazwa hadharani limeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kuitambua na kuenzi mchango wa viongozi wanaochochea maendeleo ya jamii, hususan katika sekta ya elimu.
Akizungumza katika Mahafali ya Saba ya Kidato cha Sita yaliyofanyika shuleni hapo, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Leon Malisa, alisema bodi imefikia uamuzi huo baada ya kutathmini mchango wa viongozi mbalimbali na kuona kuwa Makonda anastahili heshima hiyo.
Alifafanua kuwa mbali na wadhifa wake wa uwaziri, Makonda pia ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini na amekuwa na ushawishi mkubwa katika kusukuma mbele ajenda za maendeleo, jambo ambalo linaweza kuwa chachu kwa wanafunzi wa shule hiyo kujifunza na kuiga mifano bora ya uongozi.
“Ni muhimu kuwa na mlezi ambaye si tu ana nafasi ya uongozi, bali pia ana uwezo wa kuhamasisha, kuongoza na kuwa mfano kwa vijana wetu. Tunamwona Paul Makonda kama mtu sahihi kwa nafasi hiyo,” alisema Malisa.
Katika hatua nyingine, Malisa alieleza kuwa bodi imependekeza pia kubadilishwa kwa jina la shule hiyo kutoka “Korona” kwenda jina la Makonda, akibainisha kuwa jina la sasa linatumika na shule nyingi nchini, hali inayopunguza upekee wa taasisi hiyo.
“Tunataka shule yetu iwe na utambulisho wa kipekee na wa kuheshimika. Kumpa jina la Paul Makonda kutaleta hadhi mpya, motisha kwa wanafunzi na hata kuongeza mvuto kwa wadau wa elimu,” alisisitiza.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na wazazi, walezi, walimu pamoja na wageni mbalimbali ambapo wahitimu walitunukiwa vyeti vyao na kuagwa rasmi kuelekea hatua nyingine za elimu na maisha.
Hata hivyo, pendekezo hilo linaweza kuhitaji taratibu rasmi za kiserikali na ridhaa ya mamlaka husika kabla ya utekelezaji wake, ikiwemo Wizara ya Elimu pamoja na mamlaka nyingine zinazohusika na usajili na majina ya taasisi za elimu.
Kwa sasa, macho na masikio ya wengi yameelekezwa kuona namna ambavyo Paul Makonda atapokea pendekezo hilo, huku wadau wa elimu wakisubiri hatua zitakazofuata katika mchakato huo unaoweza kubadili historia ya shule hiyo kongwe jijini Arusha.
Ends..

0 Comments