MAKAMPUNI 100 KUSHIRIKI MAONESHO YA OSHA NJOMBE

 MAKAMPUNI 100 KUSHIRIKI MAONESHO YA OSHA NJOMBE

Arushadigital | Njombe

Zaidi ya makampuni 100, yakiwemo yanayojihusisha na sekta ya uchimbaji wa madini, yanatarajiwa kushiriki katika maonesho makubwa ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), yatakayofanyika katika viwanja vya Sabasaba mjini Njombe.

Maonesho hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Aprili 24, 2026 na kufikia kilele chake Aprili 29, sambamba na maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani, ambayo ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea kilele cha sherehe za Mei Mosi kitaifa.

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari na Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Meneja wa OSHA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Wilbert Ngowi, amesema maandalizi ya tukio hilo yamekamilika na mazingira yote yako tayari kupokea washiriki kutoka ndani na nje ya mkoa huo.

Ngowi alieleza kuwa pamoja na maonesho hayo, OSHA pia imeandaa utoaji wa tuzo maalum kwa makampuni na taasisi zitakazoonesha viwango bora vya kuzingatia masuala ya usalama na afya kazini.

Alifafanua kuwa tuzo hizo zitatolewa Aprili 29 katika ukumbi wa Agrimet mjini Njombe, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu.

Mbali na maonesho, Ngowi amesema OSHA imepanga kuendesha semina maalum kwa wafanyakazi mkoani Njombe Aprili 27, zitakazojikita katika masuala ya kazi, afya pamoja na saikolojia kazini, ikiwa ni sehemu ya kuongeza uelewa na ustawi wa wafanyakazi.

Aidha, amebainisha kuwa kutakuwa na michezo mbalimbali itakayoshirikisha wadau wa kazi na ajira, ikiwa ni njia ya kuimarisha mshikamano na afya za washiriki wakati wa maadhimisho hayo.

“Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu yanakuwa yenye mafanikio makubwa. Tunatoa wito kwa makampuni ambayo bado hayajakamilisha taratibu za ushiriki kujitokeza na kujisajili kupitia mfumo wa OSHA,” amesema Ngowi.

Kwa upande wake, Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimesema kwa mara ya kwanza mwaka huu kinashiriki maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa yanayofanyika mkoani Njombe, pamoja na kushiriki katika matukio mengine yanayoendelea katika mikoa mbalimbali nchini.

Maonesho hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kuonesha teknolojia na mbinu bora za kulinda afya na usalama wa wafanyakazi, pamoja na kuhamasisha uzingatiaji wa sheria na kanuni za kazi nchini.

MWISHO

Post a Comment

0 Comments