MFANYABIASHARA MAASAI MARKET ANUSURIKA KUUAWA KWA MAPANGA OL-MOT, POLISI WAANZA UCHUNGUZI MKALI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MFANYABIASHARA wa vinyago vya utalii katika soko maarufu la Maasai Market jijini Arusha, Isaya Mollel amenusurika kuuawa baada ya kushambuliwa kikatili kwa mapanga na watu wawili waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki katika eneo la Mtaa wa Mlimani, Kata ya Olmot, alfajiri akiwa katika mazoezi ya asubuhi pamoja na mkewe.
Tukio hilo lililotokea mapema asubuhi limetokea umbali mfupi kutoka nyumbani kwao, ambapo wanandoa hao walikuwa wameanza matembezi yao ya kawaida ya mazoezi kabla ya kuanza shughuli za siku.
SHAMBULIO LA GHAFULA NA LA KUTISHA
Akisimulia mkasa huo wa kutisha, Mollel alisema walikumbana na pikipiki iliyokuwa na watu wawili karibu na eneo la shule, ambapo ghafla waliwamulika kwa mwanga mkali wa taa za pikipiki hiyo na kuwafanya washindwe kuona kwa muda.
“Walituwashia mwanga mkali sana wa pikipiki tukapoteza uwezo wa kuona kwa sekunde chache. Tulipofumbua macho tayari walikuwa karibu sana na wakasema ‘huyu hapa’ kisha wakaanza kushambulia,” alisema Mollel.
Alieleza kuwa washambuliaji hao walimvamia moja kwa moja kwa mapanga, wakilenga miguu, mikono na kichwa, huku akijaribu kujilinda bila mafanikio na kumjeruhi vibaya mkono,Makalio na sehemu mbalimbali za mwili .
“Nilijaribu kujikinga kwa mkono wa kushoto lakini walinikata vibaya sana. Baadaye walilenga kichwani, nikauzuia tena kwa mkono huo huo ndipo wakaukata karibu na kiwiko,” alisimulia kwa majonzi.
WALIKATAA KUCHUKUA PESA, WALILENGA KUUA
Kile kilichowashangaza zaidi ni kwamba washambuliaji hao hawakuonyesha dalili yoyote ya wizi.
“Niliwaambia wachukue pesa au chochote wanachotaka waniache hai, lakini walikataa kabisa. Walikuwa wakisisitiza wanikate shingo,” alisema Mollel.
Aliongeza kuwa kutokana na giza hakuwatambua, ingawa anahisi huenda mmoja wao anafahamiana naye kutokana na sauti aliyosikia wakisema “ndiyo huyu hapa”.
MKE ASHUHUDIA MUME AKIKATWA MAPANGA ATIMUA MBIO
Mke wake, Magreth Isaya Mollel, alishuhudia tukio hilo la kinyama likitokea mbele ya macho yake kabla ya kukimbia kuomba msaada.
“Walituwashia taa kali sana, tulipofumba macho wakatufikia. Mmoja alishuka na panga akamvamia mume wangu moja kwa moja na kuanza kumkata kwa panga na mimi niliamua kukimbia kuomba msaada” alisema kwa uchungu.
Alieleza kuwa alikimbia kuelekea makazi ya karibu akipiga kelele kuomba msaada, na majirani walifika haraka eneo la tukio.
“Tuliporudi na majirani tulimkuta amelala chini amejeruhiwa vibaya, na washambuliaji walikuwa tayari wametoroka,” alisema.
HOFU YATAWALA OL-MOT
Tukio hilo limezua hofu kubwa miongoni mwa wakazi wa Olmot na wafanyabiashara wa Maasai Market, wakitaka hatua za haraka za kiusalama zichukuliwe hasa nyakati za asubuhi na jioni.
DIWANI ATOA KAULI, ATANGAZA MPANGO WA KITUO CHA POLISI
Diwani wa Kata ya Olmot, Robert Konina, amethibitisha tukio hilo na kulaani vikali shambulio hilo, akisema ni ishara ya changamoto za kiusalama zinazohitaji hatua za haraka.
“Tayari tumepokea taarifa na ni tukio la kusikitisha sana. Tumeanza hatua za kuimarisha ulinzi shirikishi na doria katika maeneo yote ya kata,” alisema.
Diwani huyo alibainisha pia kuwa serikali ya eneo hilo imeanza mchakato wa ujenzi wa kituo cha polisi katika eneo la Safari City ili kuongeza ufanisi wa kukabiliana na matukio ya uhalifu.
“Hiki kituo kitasaidia kupunguza muda wa mwitikio wa polisi na kuimarisha usalama wa wananchi,” aliongeza.
UCHUNGUZI WAANZA
Polisi wamesema wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini na kuwakamata wahusika wa shambulio hilo, huku hali ya majeruhi ikiendelea kufuatiliwa.
Hadi sasa, Isaya Mollel anaendelea kupatiwa matibabu huku familia, wafanyabiashara na wakazi wakisubiri majibu ya uchunguzi huo wa kikatili uliotikisa Olmot.
Ends..








0 Comments