UINGEREZA YAIPELEKA TANZANIA UNHRC, YATAKA UCHUNGUZI HURU KUHUSU TUHUMA ZA UKATILI BAADA YA UCHAGUZI

 UINGEREZA YAIPELEKA TANZANIA UNHRC, YATAKA UCHUNGUZI HURU KUHUSU TUHUMA ZA UKATILI BAADA YA UCHAGUZI

Na Arushadigital


Serikali ya Uingereza imeifikisha Tanzania katika mjadala wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), ikitaka kufanyika kwa uchunguzi huru, wa kina na wa uwazi kufuatia kile ilichokiita “ukatili wa kushtua” ulioripotiwa kutokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Hoja hiyo iliwasilishwa Machi 2, 2026 wakati wa mdahalo mkuu wa 61 wa Baraza hilo uliofanyika jijini Geneva, Uswizi, na Balozi wa Haki za Binadamu wa Uingereza, Eleanor Sanders. Katika hotuba yake, alieleza kuwa kuna taarifa na ushahidi unaoashiria matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwemo tuhuma za mauaji ya kinyume cha sheria na madai ya miili ya wahanga kutokuzikwa kwa heshima stahiki.

Akizungumza mbele ya wajumbe wa kimataifa, Balozi Sanders alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na ulinzi wa haki za msingi za kikatiba kwa raia wote.

“Lazima kuwepo na uchunguzi huru, wa wazi na jumuishi wa matukio haya ili kuhakikisha uwajibikaji na kulinda misingi ya utawala wa sheria na demokrasia,” alinukuliwa akisema.

Kauli hiyo imeiweka Tanzania katika shinikizo la kidiplomasia, huku Uingereza ikitumia jukwaa la UNHRC kuhoji mfululizo wa matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu yaliyoripotiwa kufuatia mchakato wa uchaguzi huo.

Tume ya Ndani Yaanza Kazi

Hatua ya Uingereza imekuja wakati ambapo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, tayari ameunda Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Tume hiyo inaendelea na vikao na mahojiano na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa sasa na wastaafu, taasisi za kiraia pamoja na wananchi, kwa lengo la kukusanya ushahidi na ushauri wa kitaalamu kuhusu matukio yaliyoripotiwa. Serikali imeeleza kuwa lengo la tume hiyo ni kubaini ukweli, kushauri hatua stahiki na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Msimamo wa Uingereza Katika Mataifa Mengine

Mbali na kuibua hoja kuhusu Tanzania, Uingereza pia ilitumia mdahalo huo kukemea ukiukwaji wa haki za binadamu katika maeneo mengine duniani. Iliitaka Israel kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia Gaza na kusitisha ujenzi wa makazi katika Ukingo wa Magharibi; iliitaka China kuachilia watu wanaodaiwa kuwekwa kizuizini kiholela katika eneo la Xinjiang na kukomesha tuhuma za ajira ya kulazimishwa; na ikaendelea kuunga mkono mamlaka ya Ukraine katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi.

Taswira ya Kimataifa

Wachambuzi wa masuala ya diplomasia wanaona hatua hiyo ya Uingereza kama ishara ya kuongezeka kwa uangalizi wa kimataifa juu ya mwenendo wa haki za binadamu barani Afrika na duniani kwa ujumla. Hata hivyo, macho ya jumuiya ya kimataifa sasa yanaelekezwa katika hatua zitakazochukuliwa na mamlaka za Tanzania—iwe ni kupitia tume ya ndani au kwa ushirikiano na taasisi za kimataifa—ili kuhakikisha ukweli unabainishwa na haki inatendeka kwa mujibu wa sheria.

Chanzo Jambo Tv

Post a Comment

0 Comments