LUKUMAY AFUNGUA MILANGO YA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KATIKA SEKTA YA AFYA
Na Joseph Ngilisho – Arusha Digital, New Delhi
MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ameendeleza jitihada za kuimarisha huduma za afya nchini baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Hospitali Bobezi ya Aakash Healthcare Super Speciality Hospital jijini New Delhi, India, Machi 3, 2026.
Katika ziara hiyo, Dkt. Lukumay alifanya mazungumzo ya kina na uongozi wa hospitali hiyo yaliyolenga kuweka msingi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya taasisi za afya za India na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kuboresha huduma za ubobezi, tafiti na mafunzo kwa watumishi wa afya.
Ushirikiano wa Ubobezi na Mafunzo
Kwa mujibu wa makubaliano ya awali, pande zote mbili zimekubaliana kushirikiana katika maeneo kadhaa muhimu, ikiwemo utoaji wa huduma za afya za kibingwa kwa wagonjwa wa Tanzania, kubadilishana utaalamu wa kitabibu, na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa Kitanzania kupitia mafunzo maalumu yatakayofanyika nchini India.
Aidha, ushirikiano huo utahusisha tafiti za pamoja kuhusu magonjwa sugu, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa kitaalamu na kuimarisha mbinu za kinga, uchunguzi na tiba kwa magonjwa yanayoendelea kuongezeka nchini.
Kliniki za Ubobezi Tanzania
Moja ya maazimio muhimu ni kuanzishwa kwa kliniki maalumu za kibingwa (specialist outreach clinics) zitakazoendeshwa kwa ushirikiano kati ya madaktari wa India na wenzao wa Tanzania katika hospitali kadhaa za rufaa.
Hospitali zitakazonufaika na mpango huo ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru na Hospitali ya Wilaya ya Olturumet.
Hatua hiyo inatarajiwa kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa matibabu ya kibingwa, kupunguza gharama kwa familia na taifa kwa ujumla, pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma bora karibu na wananchi.
Ziara ya Utekelezaji Aprili
Katika kuharakisha utekelezaji wa makubaliano hayo, viongozi waandamizi wa Hospitali ya Aakash wanatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini Tanzania mwezi Aprili 2026. Ziara hiyo itahusisha mikutano na mamlaka husika za afya kwa ajili ya kurasimisha makubaliano na kuweka mpango kazi wa utekelezaji.
Ziara ya Dkt. Lukumay inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha diplomasia ya maendeleo katika sekta ya afya, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wa Arumeru Magharibi na Watanzania kwa ujumla wananufaika na huduma za kisasa za kitabibu zenye viwango vya kimataifa.



0 Comments