NDÚVA AAGA RASMI UONGOZI EAC, ATAJA MAFANIKIO YA MIEZI 20

 NDÚVA AAGA RASMI UONGOZI EAC, ATAJA MAFANIKIO YA MIEZI 20

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


KATIBU Mkuu anayemaliza muda wake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Veronica Nduva, ameaga rasmi uongozi wa jumuiya hiyo akieleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miezi 20 aliyohudumu, huku akisisitiza kuwa EAC inaendelea kuwa imara licha ya changamoto za kifedha na kisiasa.

Akizungumza wakati wa mkutano maalumu wa Wakuu wa Nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha, Nduva aliwashukuru viongozi wa nchi wanachama kwa ushirikiano na mwongozo waliompa katika kipindi chote cha uongozi wake.

Alisema ushirikiano huo ulimwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kipindi ambacho jumuiya hiyo ilikuwa inapitia changamoto mbalimbali za kiutawala, kifedha na rasilimali watu.

“Hii ni fursa yangu ya mwisho kuwahutubia Waheshimiwa kama Katibu Mkuu wenu katika mkutano wa kilele. Napenda kuwashukuru kwa dhati kwa mwongozo, ushirikiano na kwa kunipokea kila nilipohitaji kukutana nanyi kujadili masuala ya jumuiya yetu,” alisema Nduva.

Alibainisha kuwa alipoingia madarakani, EAC ilikuwa katika kipindi nyeti ikikabiliwa na changamoto za uaminifu wa taasisi, uhaba wa fedha pamoja na upungufu wa rasilimali watu, hali iliyomlazimu kuweka vipaumbele katika kuimarisha taasisi na kurejesha imani ya wananchi kwa jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa Nduva, katika kipindi cha uongozi wake EAC imepiga hatua kadhaa muhimu ikiwemo kuongezeka kwa biashara za mipakani zinazofanywa na wanawake, hususan katika sekta ya biashara ndogo, ndogo na za kati.

Aidha alisema idadi ya wanafunzi wanaovuka mipaka ya nchi wanachama kwenda kusoma katika mataifa mengine ya jumuiya hiyo imeongezeka, hatua inayochochea zaidi mshikamano na ushirikiano wa kikanda.

Katibu Mkuu huyo pia alieleza kuwa katika kipindi hicho, EAC imefanikiwa kuongeza ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika mijadala ya maendeleo ya jumuiya hiyo wakiwemo sekta binafsi, vijana, wanawake, wanafunzi pamoja na mashirika ya kiraia.

Aliongeza kuwa jumuiya hiyo pia imeimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali na kuongeza uwepo wake katika majukwaa ya mtandao, hatua inayoiweka EAC kuwa miongoni mwa jumuiya za kikanda barani Afrika zinazoongoza katika kukuza mazingira ya kidijitali yaliyo wazi na salama kwa wananchi wake.

Katika hatua nyingine, Nduva alisema uwajibikaji na weledi ndani ya taasisi na vyombo vya jumuiya hiyo umeimarishwa kupitia kuanzishwa kwa mifumo madhubuti ya udhibiti wa ndani pamoja na maboresho ya taratibu za kiutawala.

Pia alibainisha kuwa EAC imeongeza ushirikiano na washirika wa maendeleo, jambo lililosaidia kuongezeka kwa msaada wa kitaalamu na kifedha katika utekelezaji wa programu mbalimbali zinazowanufaisha wananchi wa nchi wanachama.

“Ninapenda kuwashukuru washirika wa maendeleo ambao wameendelea kuwa na imani na uwezo wa taasisi zetu kwa kutoa msaada wa moja kwa moja wa kifedha katika utekelezaji wa shughuli za jumuiya,” alisema.

Akihitimisha hotuba yake, Nduva aliwapongeza watumishi wa taasisi na vyombo vya EAC kwa kujituma na kuendeleza agenda ya ushirikiano wa kikanda, huku akilitambua pia Baraza la Mawaziri wa EAC kwa mwongozo wa sera na ushirikiano wao katika kuendeleza malengo ya jumuiya.

Alisisitiza kuwa licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza, jumuiya hiyo inaendelea kuwa imara na iko katika mwelekeo sahihi wa kufikia malengo na matarajio yaliyowekwa katika mkataba wa kuanzishwa kwake.

“Nina imani kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kuwa thabiti na kufikia malengo yake ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa manufaa ya wananchi wa ukanda huu,” alisema.

Nduva aliwatakia Wakuu wa Nchi wa EAC majadiliano yenye tija katika mkutano huo na kueleza matumaini yake kuwa maamuzi yatakayofikiwa yataongeza kasi ya utekelezaji wa malengo ya jumuiya hiyo.

ENDS..

Post a Comment

0 Comments