Biashara ya EAC Yapaa Hadi Dola Bilioni 40.3
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
BIASHARA ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeendelea kushuhudia ukuaji wa ajabu, ikifikia dola za Marekani bilioni 40.3 katika robo ya tatu ya mwaka 2025, ongezeko la asilimia 21.9 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Hayo yamebainika katika ripoti ya Baraza la Mawaziri la EAC iliyosomwa na mwenyekiti wa Baraza hilo Bi. Beatrice Askui, wakati wa Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi za EAC jijini Arusha huku ripoti hiyo ikipita bila kupingwa.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa ukuaji huu umechangiwa zaidi na ongezeko la mauzo ya nje (exports) ya nchi wanachama, ambayo yameongezeka kwa asilimia 32.3.
Hali kadhalika, uagizaji bidhaa kutoka nje (imports) uliongezeka kwa asilimia 13.3 pekee, hatua iliyosaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa pengo la nakisi ya biashara katika ukanda.
Aidha, biashara kati ya nchi wanachama wa EAC imeimarika, ikiongezeka kwa asilimia 15 kutoka dola bilioni 4.3 hadi dola bilioni 4.8 katika kipindi hicho.
Ukuaji huu unaonyesha juhudi endelevu za nchi wanachama kuimarisha biashara ya kikanda na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi ndani ya jumuiya.
Jumuiya ya EAC imeendelea kusogeza mbele utengenezaji na urahisishaji wa biashara kupitia utekelezaji wa Single Customs Territory, ikiwemo kuanzishwa rasmi kwa East Africa Customs Bond.
Mfumo huu mpya unatarajiwa kuachia zaidi ya dola bilioni 2 ambazo awali zilikuwa zimefungwa kama mitaji ya kazi katika mifumo tofauti ya dhamana za kitaifa, huku pia ukipunguza gharama za utawala na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa.
Aidha, juhudi za kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru zinaendelea, hatua inayosaidia kupunguza ucheleweshaji wa bidhaa mipakani na kuboresha mazingira ya biashara.
EAC pia imeendeleza maonyesho ya Micro, Small and Medium Enterprises Trade Fair yaliyofanyika Nairobi kuanzia Novemba 5–16, 2025, yakiwakutanisha zaidi ya waoneshaji 2,000 kutoka nchi wanachama, na kutoa fursa kubwa za biashara na ubia wa kibiashara.
Kwenye uwekezaji, jumuiya hiyo imepitisha kanuni za pamoja za kuoanisha sheria za uwekezaji ili kurahisisha nchi wanachama kulinganisha mifumo yao ya kitaifa na kuboresha mazingira ya biashara.
Katika usafiri wa anga, EAC imezindua East Africa Centre for Aviation Medicine jijini Nairobi, kwa ushirikiano na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Kenya (KCAA), kituo kitakachosaidia kusimamia viwango vya afya kwa wahudumu wa anga.
EAC pia imeanzisha chapa mpya ya utalii ya kikanda, “Visit East Africa”, iliyozinduliwa katika maonesho ya kimataifa ya utalii nchini Ubelgiji Machi 2025, kwa lengo la kuiweka Afrika Mashariki kama kituo kimoja cha utalii duniani na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea ukanda.
Kwenye afya, jumuiya hiyo imeandaa mfumo wa kikanda wa kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na milipuko ya magonjwa ili kuimarisha uthabiti wa mifumo ya afya ya umma katika nchi wanachama.
Kwenye muungano wa fedha, EAC inaendelea kutekeleza ramani ya kuanzishwa kwa East African Monetary Union, pamoja na kuratibu sera za fedha, bajeti, na mpango mkuu wa malipo mipakani.
Aidha, jumuiya inashughulikia rasimu ya katiba ya Political Confederation na kushiriki katika juhudi za amani na usalama, ikiwemo mchakato wa Nairobi wa kurejesha amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
EAC imekamilisha mkakati wake wa maendeleo wa miaka saba (2023–2027), unaolenga kujenga jumuiya iliyo unganishwa, imara na yenye ustahimilivu wa kiuchumi, kwa manufaa ya wananchi wa Afrika Mashariki.
Ukuaji huu unaonesha wazi kuwa EAC ipo katika njia thabiti ya kuwa kiini cha biashara, uwekezaji, utalii, na maendeleo endelevu katika bara la Afrika.
Ends

0 Comments