MJOMBA ALIYEMPIGA MTOTO NA KUMNING'INIZA KIKATILI DIRISHANI AROBAINI ZAKE HIZI HAPA..

 MJOMBA AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUMNING’INIZA MTOTO DIRISHANI TABORA

Na Arushadigital |TABORA

Jeshi la Polisi nchini linamshikilia mtu mmoja aitwaye Joseph Mbalamwezi Francis, mkazi wa Mtaa wa Imalamakoe B, Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora, kwa tuhuma za kumfanyia ukatili mtoto wa miaka 10 kwa kumfunga kamba mikononi na miguuni kisha kumning’iniza dirishani.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano, Machi 4, 2026, na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu tukio hilo lililotokea Machi 2, 2026.

Kwa mujibu wa DCP Misime, mtoto huyo ambaye ni mpwa wa mtuhumiwa alikuwa akiishi katika nyumba moja na mjomba wake huyo kabla ya tukio hilo la kikatili kutokea.

Alieleza kuwa taarifa za awali zinaonyesha mtuhumiwa alidai kumwadhibu mtoto huyo baada ya kuunguza mboga aina ya nyama aliyokuwa akipika, jambo lililodaiwa kumkasirisha na kumpelekea kumfanyia adhabu kali isiyokubalika kisheria wala kijamii.

“Inadaiwa mtoto huyo alipigwa na kisha kufungwa kamba mikononi na miguuni kabla ya kuning’inizwa dirishani. Hata hivyo, alifanikiwa kuokolewa na kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu,” alisema DCP Misime.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi huku hatua za kisheria zikiendelea kuchukuliwa dhidi yake.

Aidha, Polisi wamewashukuru wananchi waliotoa taarifa kwa wakati ambazo zilisaidia kuokoa maisha ya mtoto huyo na kuwezesha kukamatwa kwa mtuhumiwa.

Jeshi hilo pia limetoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kupinga na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto, likisisitiza kuwa ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu la kila mwanajamii.

Post a Comment

0 Comments