MBUNGE LUKUMAY AZIDI KUCHANJA MBUGA ,AFUNGUA MILANGO YA USHIRIKIANO NA INDIA KUIMARISHA HUDUMA ZA SARATANI TANZANIA

 LUKUMAY AFUNGUA MILANGO YA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KUIMARISHA HUDUMA ZA SARATANI TANZANIA

Na Joseph Ngilisho | Arushadigital |INDIA


MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi,Mkoani Arusha Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ameendeleza jitihada za kutafuta ushirikiano wa kimataifa wa kuboresha huduma za afya nchini baada ya kufanya ziara katika Rajagiri Hospital iliyopo Jimbo la Kerala kusini mwa India.

Ziara hiyo iliyofanyika Machi 5, 2026 imelenga kujifunza na kujadiliana namna bora ya kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika tiba ya saratani na magonjwa mengine makubwa nchini Tanzania, sambamba na kuangalia fursa za mafunzo kwa wataalamu wa afya.

Hospitali ya Rajagiri inatajwa kuwa miongoni mwa vituo vya afya vilivyoendelea kiteknolojia nchini India, ikiwa imebobea katika matumizi ya vifaa tiba vya kisasa ikiwemo teknolojia ya PET Scan pamoja na matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI) katika uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali ya binadamu.

Katika ziara hiyo, Dkt. Lukumay alifanya kikao cha majadiliano na uongozi wa hospitali hiyo kujadili uwezekano wa kusaidia kuimarisha uwezo wa hospitali mbili muhimu nchini Tanzania ambazo ni Ocean Road Cancer Institute pamoja na Olturumet District Hospital.


Kwa mujibu wa Dkt. Lukumay, hospitali ya Ocean Road imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za saratani baada ya serikali kununua mashine ya kisasa ya PET Scan ambayo hutumika kugundua saratani mapema na kufuatilia maendeleo ya matibabu kwa usahihi mkubwa.

Alieleza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya maboresho makubwa ya sekta ya afya yanayotekelezwa na serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo zaidi ya shilingi trilioni 6.7 zimeelekezwa katika kuimarisha miundombinu ya afya, kununua vifaa tiba vya kisasa na kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.


“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, na sasa kinachohitajika zaidi ni kuhakikisha wataalamu wetu wanapata mafunzo ya kutosha kutumia teknolojia hizi za kisasa ili wananchi wanufaike kikamilifu,” alisema Dkt. Lukumay.

Kwa upande wa Olturumet District Hospital, hospitali hiyo tayari ina mashine ya Mammography inayotumika kuchunguza saratani ya matiti, huduma ambayo imeanza kusaidia wanawake wengi katika kugundua ugonjwa huo mapema.

Katika kikao hicho, pande zote zilikubaliana kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ili kuwezesha wataalamu wa afya kutoka hospitali za Ocean Road na Olturumet kwenda India kupata mafunzo maalum ya matumizi ya mashine za PET Scan na Mammography.



Aidha, madaktari bingwa kutoka Rajagiri Hospital watatembelea Tanzania kutoa mafunzo ya vitendo kwa watumishi wa afya wanaotumia vifaa hivyo pamoja na teknolojia nyingine za kisasa zilizonunuliwa na serikali.

Katika hatua nyingine ya kuimarisha ushirikiano huo, viongozi waandamizi wa Rajagiri Hospital wanatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini Tanzania mwezi Aprili 2026, ambapo watatembelea taasisi mbalimbali ikiwemo Ocean Road, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI pamoja na Halmashauri ya Arusha.

Ziara hiyo inatarajiwa kuwa mwanzo wa ushirikiano mpana wa kitaalamu kati ya Tanzania na India katika sekta ya afya, hususan katika mapambano dhidi ya saratani na matumizi ya teknolojia za kisasa katika tiba.

Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za afya nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu ya kisasa ndani ya nchi bila kulazimika kusafiri nje ya Tanzania.










 

Ends

Post a Comment

0 Comments