MAZISHI YA KITAIFA YA KIONGOZI MKUU WA IRAN YAHAIRISHWA; MAANDALIZI YAENDELEA WAKATI MVUTANO WA KIJESHI UKIONGEZEKA
Na Arushadigital
Mazishi ya kitaifa ya Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Machi 4, yameahirishwa kwa muda usiojulikana huku maandalizi ya tukio hilo yakionekana kuendelea katika maeneo mbalimbali nchini humo.Picha na video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha shughuli za maandalizi zikiendelea, zikiwemo uwekaji wa miundombinu ya mapokezi ya maelfu ya waombolezaji pamoja na hatua za kuimarisha usalama katika maeneo yanayotarajiwa kutumika kwa shughuli za mazishi.
Hadi sasa, Serikali ya Iran haijatoa tamko rasmi linaloeleza sababu za kuahirishwa kwa mazishi hayo ya kitaifa. Hata hivyo, duru mbalimbali za habari zinadokeza kuwa uamuzi huo unaweza kuwa umechochewa na masuala ya kiusalama, upangaji wa maandalizi ya kitaifa pamoja na hali ya kisiasa inayozidi kuwa tete katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kifo cha Ayatollah Khamenei, ambaye aliongoza Iran kwa zaidi ya miongo kadhaa akiwa mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika siasa na dini ya Kiislamu ya madhehebu ya Shia, kimeibua mjadala mpana ndani na nje ya nchi kuhusu mustakabali wa uongozi wa juu wa taifa hilo pamoja na mwelekeo wa kisiasa wa Iran katika kipindi kijacho.
Wachambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa wanaeleza kuwa pengo la uongozi lililoachwa na kifo chake linaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa sera za ndani na za nje za Iran, hasa katika kipindi ambacho nchi hiyo inakabiliwa na changamoto za kiusalama na mvutano wa kikanda.
Wakati huo huo, hali ya usalama katika Mashariki ya Kati imeendelea kuwa tete kufuatia kuendelea kwa mapigano kati ya Israel na Iran, ambayo sasa yameingia siku ya tano mfululizo. Jeshi la Israel limetangaza kuanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya anga na makombora katika maeneo kadhaa ya kimkakati, hatua inayodaiwa kulenga kudhoofisha miundombinu ya kijeshi ya Iran na washirika wake katika ukanda huo.
Mvutano huo umeibua hofu ya kuongezeka kwa mgogoro mpana wa kijeshi katika Mashariki ya Kati, huku jumuiya ya kimataifa ikitoa wito wa tahadhari na juhudi za haraka za kidiplomasia ili kuzuia kuzorota zaidi kwa hali ya usalama.
Kwa sasa, Serikali ya Iran inatarajiwa kutangaza tarehe mpya ya mazishi ya kitaifa ya kiongozi huyo mara baada ya kukamilika kwa maandalizi muhimu pamoja na tathmini ya kina ya hali ya usalama kwa lengo la kuhakikisha tukio hilo linafanyika kwa utulivu na usalama wa umma.
Ends

0 Comments