MARAIS WA EAC KUKUTANA ARUSHA, KUZINDUA HATI MUHIMU ZA UCHUMI NA KUAMUA UONGOZI MPYA
Na Joseph Ngilisho|ARUSHA
Marais wanane wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) wanatarajiwa kukutana Machi 7, 2026 katika Mkutano wa 25 wa Kilele, wakitarajiwa kufanya maamuzi mazito yatakayogusa mustakabali wa kiuchumi, kisiasa na kisheria wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika mkutano huo, Wakuu wa Nchi wanatarajiwa kuzindua nyaraka mbili zenye uzito wa kimkakati, ikiwamo Dhamana ya Forodha ya Jumuiya (EAC Customs Bond), hatua inayolenga kurahisisha usafirishaji wa mizigo mipakani, kupunguza urasimu na kuongeza ufanisi wa biashara ndani ya soko la pamoja la kikanda.
Sambamba na hilo, viongozi hao watazindua Mkakati wa Saba wa Maendeleo wa Jumuiya (7th EAC Development Strategy), ambao utaweka mwelekeo wa miradi ya kimkakati, uwekezaji na mageuzi ya kiuchumi kwa kipindi kijacho, kwa lengo la kuimarisha ushindani wa Jumuiya katika ngazi ya bara na kimataifa.
Akizungumza March 3,2026 na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva, alisema mkutano huo ni wa kikatiba na hufanyika kila mwaka kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzilishi wa EAC, ukiwa ni chombo cha juu kabisa cha maamuzi ndani ya Jumuiya.
“Huu ni Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi tangu kufufuliwa kwa Jumuiya. Awali ulipangwa kufanyika Novemba 2025, lakini ukaahirishwa kupisha Uchaguzi Mkuu wa Tanzania. Sasa maandalizi yamekamilika,” alisema Nduva.
Mbali na uzinduzi wa nyaraka hizo, ajenda nyingine kuu ni mabadiliko ya uongozi katika ngazi za juu za Jumuiya. Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, Ofisi ya Mwenyekiti wa EAC hubadilishwa kila mwaka kwa mzunguko wa nchi wanachama.
Kwa sasa, nafasi hiyo inashikiliwa na Rais wa Kenya, William Ruto, ambaye atawasilisha ripoti ya utekelezaji wa majukumu yake kama Mwenyekiti kabla ya kukabidhi kijiti kwa kiongozi atakayechaguliwa kwa makubaliano ya Wakuu wa Nchi.
“Marais wataketi na kuafikiana juu ya nani atakayechukua nafasi ya Mwenyekiti kwa mwaka unaofuata,” alieleza Nduva.
Aidha, mkutano huo utaamua hatima ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa EAC. Kwa mujibu wa utaratibu wa mzunguko wa nchi wanachama, nafasi hiyo hubadilishwa kila baada ya miaka mitano. Kenya imekuwa na nafasi hiyo tangu mwaka 2021 hadi 2026, na sasa Wakuu wa Nchi wanatarajiwa kujadili na kuteua Katibu Mkuu mpya atakayeongoza Sekretarieti kwa muhula ujao.
Katika hatua nyingine, Wakuu wa Nchi wataapisha majaji wapya wa Mahakama ya Haki ya Afrika ya Mashariki (EACJ), chombo kinachosimamia tafsiri na utekelezaji wa sheria za Jumuiya.
Vilevile, watajadili taarifa ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa katika Mkutano wa 24 wa Kilele wa mwaka 2024, pamoja na tathmini ya mafanikio na changamoto katika sekta za biashara, miundombinu, amani na usalama.
Zaidi ya wajumbe 700 kutoka nchi wanachama wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo, wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu wa wizara husika na wadau wengine wa kikanda.
Kwa mujibu wa Nduva, ngazi za kitaalamu tayari zimeanza vikao vya maandalizi, vikihakiki ripoti na mapendekezo yatakayowasilishwa kwa Baraza la Mawaziri na hatimaye kwa Wakuu wa Nchi kwa uamuzi wa mwisho.
Mkutano huo unatazamwa kuwa wa maamuzi mapana katika kipindi ambacho Jumuiya inaendelea kupanuka na kukabiliwa na matarajio makubwa ya wananchi wake katika kuimarisha uchumi wa pamoja na ushirikiano wa kikanda.





0 Comments