Lukumay Afungua Milango ya Ushirikiano wa Kimataifa Kuboresha Huduma za Afya Arumeru
Na Joseph Ngilisho- INDIA
MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ameendeleza jitihada za kuimarisha sekta ya afya katika jimbo lake baada ya kufanya ziara maalumu katika Hospitali ya PSRI Hospital iliyopo New Delhi, India, na kufanya kikao cha kimkakati na uongozi wa hospitali hiyo tarehe 3 Machi, 2026.
Katika kikao hicho, pande zote mbili ziliazimia kuanzisha ushirikiano wa moja kwa moja utakaolenga kuinua kiwango cha huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya ya Olturumet kupitia mpango wa pamoja utakaoishirikisha Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.
Dawa, Vifaa Tiba na Mafunzo kwa Watumishi
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Hospitali ya PSRI itatoa usaidizi katika upatikanaji wa dawa na vifaa tiba muhimu kwa Hospitali ya Olturumet, hatua inayotarajiwa kupunguza changamoto za uhaba wa vifaa na kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, ushirikiano huo utahusisha utoaji wa mafunzo maalumu kwa watumishi wa afya ili kuwajengea uwezo wa kitaaluma, sambamba na kubadilishana watumishi kati ya hospitali hizo mbili kwa lengo la kupata uzoefu na maarifa mapya katika taaluma ya tiba na usimamizi wa hospitali.
Tafiti za Magonjwa Yasiyoambukiza
Katika kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na saratani, pande hizo zimekubaliana kuanzisha tafiti za pamoja zitakazosaidia kubaini ukubwa wa tatizo katika jamii na kuweka mikakati madhubuti ya kinga na tiba.
Hatua hiyo inaakisi mwelekeo wa kimataifa wa kuwekeza katika tafiti na kinga, hasa katika ngazi ya huduma za afya ya msingi (PHC), ambayo imepewa kipaumbele katika makubaliano hayo.
Kuimarisha PHC na Kliniki za Mikoba
Mbali na tafiti na mafunzo, ushirikiano huo utaimarisha huduma za afya ya msingi (Primary Health Care – PHC) pamoja na kuendesha kliniki za mikoba zitakazowafikia wananchi vijijini na maeneo yenye changamoto ya miundombinu ya afya.
Mpango huo unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kupunguza gharama za matibabu na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa makundi maalumu wakiwemo wazee, watoto na wajawazito.
Ziara ya Viongozi Waandamizi Tanzania
Katika hatua ya kuendeleza makubaliano hayo, viongozi waandamizi wa Hospitali ya PSRI wanatarajiwa kufanya ziara nchini Tanzania mwezi Juni, 2026, hususan katika halmashauri husika, kwa lengo la kukutana na viongozi katika ngazi mbalimbali za Serikali ili kuweka mikakati ya utekelezaji wa makubaliano hayo.
Ziara hiyo inatarajiwa kuwa chachu ya kuanza rasmi utekelezaji wa ushirikiano huo wa kimataifa, ambao ukitekelezwa kikamilifu unaweza kuwa mfano wa mafanikio katika kuunganisha rasilimali na utaalamu wa kimataifa kwa manufaa ya wananchi wa Arumeru Magharibi na Taifa kwa ujumla.
Kwa ujumla, hatua ya Dkt. Lukumay inaonekana kufungua ukurasa mpya wa diplomasia ya maendeleo katika sekta ya afya, ikilenga kuleta mageuzi ya huduma za tiba katika ngazi ya wilaya kupitia ushirikiano wa kitaalamu na taasisi zenye uzoefu wa kimataifa.
Ends .


0 Comments