CRDB na REDEOA Waingia Mashirikiano Kuimarisha Ustawi wa Maofisa Elimu
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
KATIKA hatua ya kuimarisha ustawi wa watumishi wa sekta ya elimu, CRDB Bank imesaini makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitano na Umoja wa Maofisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania Bara (REDEOA), yakilenga kuwajengea maofisa elimu uwezo wa kiuchumi kupitia huduma za kifedha na programu za mafunzo
Makubaliano hayo yalitangazwa wakati wa Mkutano Mkuu wa 12 wa REDEOA unaofanyika jijini Arusha, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, alisema mpango huo umebuniwa kwa kuzingatia nafasi muhimu ya maofisa elimu katika kusimamia na kuendeleza ubora wa elimu nchini.
Alieleza kuwa chini ya ushirikiano huo, wanachama wa REDEOA watanufaika na mikopo nafuu, mitaji wezeshi na mafunzo maalum ya ujasiriamali pamoja na elimu ya fedha itakayowasaidia kupanga, kuwekeza na kusimamia rasilimali zao kwa ufanisi.
“Tunataka kuona maofisa elimu wanapanua wigo wa kipato chao kupitia miradi halali ya kiuchumi. Tutatoa mafunzo ya kina kuhusu usimamizi wa fedha, uwekezaji na matumizi sahihi ya mikopo ili kuhakikisha wanufaika wanapata matokeo chanya,” alisema Mwambapa
Alibainisha kuwa benki hiyo pia itaendelea kushirikiana na sekta ya elimu kupitia miradi ya kijamii, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya shule, utoaji wa samani za shule, miradi ya maji na kampeni za utunzaji wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika maendeleo ya jamii.
Kwa mujibu wa Mwambapa, mafanikio ya utekelezaji wa makubaliano hayo yatapimwa kwa kuzingatia ongezeko la miradi ya kiuchumi miongoni mwa maofisa elimu na ustawi wao kwa ujumla, huku uwezekano wa kuongeza muda wa ushirikiano huo ukiwa wazi endapo malengo yatafikiwa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Elimu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dk. Emmanuel Shindika, aliipongeza CRDB kwa kuonyesha imani kwa maofisa elimu kwa kuwapatia fursa za kifedha zitakazowawezesha kujiongezea kipato na kuimarisha hadhi yao kiuchumi.
Alisema uwezeshaji huo ni sehemu ya juhudi za kujenga sekta ya elimu iliyo imara, kwani walimu na wasimamizi wa elimu wanapokuwa na utulivu wa kiuchumi, huongeza tija katika majukumu yao ya kila siku.
Naye Mwenyekiti wa REDEOA, Martin Nkwabi, alisema makubaliano hayo yamekuja wakati muafaka, akieleza kuwa wanachama wa umoja huo wamekuwa wakihitaji jukwaa la kuaminika la kifedha litakalowawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali.
Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za fedha na sekta ya elimu ni daraja muhimu la kufanikisha maendeleo endelevu, akibainisha kuwa mpango huo utasaidia pia kukuza matumizi ya TEHAMA katika huduma za kifedha na usimamizi wa miradi.
Kupitia makubaliano hayo, wadau wanaamini kuwa maofisa elimu watanufaika si tu kwa kupata mikopo, bali pia kwa kujengewa utamaduni wa kuwekeza, kuweka akiba na kupanga maendeleo yao ya muda mrefu—hatua inayotarajiwa kuwa chachu ya mageuzi chanya katika sekta ya elimu nchini.
Ends..



















0 Comments