MAFWELE BAADA YA KUZUSHIWA MAMBO YA HOVYO MTANDAONI AIBUKIA KWA POLISI KATA

 By ArushaDigital-Dar

MAFWELE AWATAKA POLISI KATA KUENDELEZA USHIRIKIANO NA JAMII



Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Faustine Mafwele amewataka Polisi Kata kuendeleza ushirikiano na jamii zilizopo katika Kata zao kwani kupitia ushirikiano huo kutaliwezesha Jeshi la Polisi kupata taarifa za uhalifu mapema kabla haujatendeka na kuchukua hatua. 


Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 02 Machi, 2026 katika bwalo la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam lililopo barabara ya Kilwa Temeke alipokuwa akizungumza na Polisi Kata 102 kutoka Mikoa ya Kipolisi Ilala, Kinondoni na Temeke kwa ajili ya kuboresha utendaji na kuleta matokeo chanya ya falsafa ya Polisii jamii.


SACP Mafwele amesema “kwanza kabisa niwatake Polisi Kata wote kuzijua vizuri Kata zenu kwa kutambua mipaka ya kijiografia, shughuli za kiuchumi zinazofanywa katika eneo lako sambamba na kutambua makundi yote muhimu yaliyopo katika maeneo yenu kwani kupitia ushirikiano na makundi hayo kutawasaidia kupata taarifa mbalimbali ikiwemo taarifa za uhalifu ambazo zitatumiwa na Jeshi la Polisi kudhibiti matukio ya kihalifu katika maeneo hayo”.


Pia SACP Mafwele amewataka Polisi Kata hao kutumia vizuri nafasi walizopewa za kufanya kazi karibu na jamii kwani kutawasaidia kutengeneza fursa za kiuchumi kulingana na sehemu walipo sambamba na kuwataka kujenga uaminifu kwa jamii hizo kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ili wanachi hao waweze kutoa taarifa mbalimbali ikiwemo taarifa za ukatili.


Aidha kwa upande wake Mkuu wa Operesheni Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) James Chacha amewakumbusha Polisi Kata hao kutambua kuwa Polisi Jamii ndio msingi mzuri katika kupambana na uhalifu na kujenga taswira nzuri ya Jeshi la Polisi katika jamii zao.


Pia Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ally Wendo amewataka Polisi Kata hao kuendelea kufanya vikao na mikutano katika Kata zao kwa ajili ya kushauri mambo yote yanayohusu usalama wa raia na mali zao.



Post a Comment

0 Comments