MAKONDA ASISITIZA UTAMBUZI WA VIPAJI KUINUA THAMANI YA MICHEZO NCHINI

 MAKONDA ASISITIZA UTAMBUZI WA VIPAJI KUINUA THAMANI YA MICHEZO NCHINI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesisitiza umuhimu wa kutambua na kukuza vipaji vya Watanzania kama njia ya kuongeza thamani ya michezo na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya taifa.

Akizungumza katika Kikao Kazi cha Maafisa Michezo kilichofanyika katika ukumbi wa Arusha International Conference Centre (AICC), Makonda alisema kuwa uwekezaji katika vipaji ni msingi muhimu wa kujenga sekta ya michezo yenye ushindani na tija, huku akibainisha kuwa taifa lina rasilimali kubwa ya vijana wenye uwezo ambao haujaendelezwa ipasavyo.

Alieleza kuwa utambuzi wa mapema wa vipaji, uwekezaji katika mafunzo na mi undombinu, pamoja na usimamizi thabiti wa programu za michezo, ni mambo yatakayochochea mafanikio ya sekta hiyo na kuiwezesha Tanzania kushindana kimataifa.

“Tunapaswa kubadili mtazamo na kuweka nguvu katika kuibua vipaji vya vijana wetu. Huko ndiko kunakoweza kuongeza thamani ya michezo yetu na kuifanya kuwa sekta yenye mchango mkubwa kiuchumi na kijamii,” alisema Makonda.

Aidha, aliwataka maafisa michezo na watumishi wa sekta hiyo kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na uzalendo, wakihakikisha wanatumia nafasi zao kuibua na kukuza vipaji katika ngazi zote kuanzia jamii hadi taifa.

Makonda alisisitiza kuwa sekta ya michezo ina uwezo mkubwa wa kuleta ajira, kukuza vipato na kuimarisha mshikamano wa kitaifa, endapo itawekewa mikakati madhubuti na kusimamiwa kwa ufanisi.

Pia alihimiza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali ili kuongeza uwekezaji katika michezo, hususan katika maeneo ya mafunzo, mashindano na uendelezaji wa vipaji.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hizo zitasaidia kujenga kizazi cha wanamichezo wenye uwezo, nidhamu na ushindani wa kimataifa, huku zikichangia katika kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya michezo.

Ends .

Post a Comment

0 Comments