WAJUMBE TASOA WATINGA ARUSHA KWA KISHINDO, WAFANYA JOGGING YA NGUVU AICC KUELEKEA MKUTANO MKUU

 WAJUMBE TASOA WATINGA ARUSHA, WAFANYA JOGGING YA KUVUTIA KUELEKEA MKUTANO MKUU

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Wajumbe wa Chama cha Maafisa Michezo Tanzania (TASOA) kutoka mikoa mbalimbali nchini wameanza kwa kishindo maandalizi ya Mkutano Mkuu wao kwa kushiriki jogging ya nguvu na mbio za kilometa tano katikati ya jiji la Arusha, tukio lililojaa hamasa, mshikamano na ari ya michezo.

Mazoezi hayo yamefanyika ikiwa ni sehemu ya kujiweka sawa kimwili na kiakili kabla ya mkutano huo muhimu unaotarajiwa kufanyika rasmi Machi 30, 2026 katika ukumbi wa kisasa wa Arusha International Conference Centre (AICC).

Tukio hilo lilianza katika viwanja vya AICC, ambapo wajumbe hao walikusanyika pamoja na vikundi mbalimbali vya mazoezi ya viungo kutoka ndani ya jiji la Arusha. Kwa pamoja, walishiriki mazoezi ya awali kabla ya kuanza mbio hizo zilizoambatana na shamrashamra za aina yake.


Wakiongozwa na gari la polisi kwa ajili ya usalama, washiriki hao walikimbia katika barabara kuu za jiji hilo huku wakivutia macho ya wakazi waliokuwa wakishuhudia tukio hilo la kipekee. Baada ya kumaliza mbio hizo, walirejea AICC na kuhitimisha kwa mazoezi mepesi ya viungo, wakichagizwa na burudani ya muziki kutoka gari la matangazo lililokuwa likiongeza hamasa kwa washiriki wote.

Miongoni mwa washiriki wa zoezi hilo alikuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo kutoka ofisi ya waziri Mkuu TAMISEMI , Yusuphu Singo ambaye alionesha kuridhishwa na ushiriki mkubwa na maandalizi yanayoendelea kuelekea mkutano huo.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Singo alisifu juhudi za wizara pamoja na uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa kuweka mazingira bora ya kufanikisha mkutano huo mkubwa wa kitaifa. Alisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha sekta ya michezo nchini, hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaendelea kujiandaa kwa mashindano makubwa ya AFCON.

Aidha, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pamoja na wizara ya Habari, Utamaduni sanaa na michezo, kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya michezo, hatua ambayo imekuwa chachu ya maendeleo na mafanikio katika tasnia hiyo.

Jogging hiyo si tu imeonesha mshikamano wa maafisa michezo nchini, bali pia imekuwa ishara ya utayari wao wa kujadili mustakabali wa michezo nchini kupitia mkutano mkuu ujao—mkutano unaotarajiwa kuibua mikakati mipya, ubunifu na dira ya maendeleo ya michezo Tanzania.









Ends..

Post a Comment

0 Comments