DC KARATU ADAIWA KUWASWEKA NDANI WAANDISHI WA HABARI WALIOANDIKA TAARIFA AMBAYO HAIKUMPENDEZA, YEYE ADAI AMEWASAMEHE

 WAANDISHI WA HABARI WAKAMATWA KWA AMRI YA DC, WAZUA MASWALI YA UHURU WA HABARI

Na Joseph Ngilisho | KARATU

Waandishi wa habari wawili wa Kituo cha Redio cha Lumen FM kilichopo wilayani Karatu, Nobert Hongoli na Wolter John Mbaga (Mhariri), wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kufuatia agizo la Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Lameck Karanga, hatua iliyozua mjadala mpana kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini.


Waandishi wanaodaiwa kusukumwa ndani kwa Amri ya DC

Tukio hilo limetokea asubuhi ya leo, Machi 27, 2026, baada ya waandishi hao kuitwa ofisini kwa Mkuu wa Wilaya kwa maelezo, kabla ya kuamriwa kukamatwa na kupelekwa kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, waandishi hao wanadaiwa kuchapisha na kurusha habari inayodaiwa “kuleta taharuki kwa jamii”, habari iliyohusu hofu ya wananchi juu ya uwezekano wa kutokea mafuriko kufuatia bwawa kujaa maji kupita kiasi. Wananchi katika eneo hilo walikuwa wakiiomba Serikali kuchukua hatua za tahadhari ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkuu wa Wilaya, Lameck Karanga, amedai kuwa mamlaka ya kutoa taarifa rasmi kuhusu hali ya maafa kama mafuriko ipo chini ya ofisi yake, na siyo vyombo vya habari kutoa taarifa hizo bila uthibitisho kutoka serikalini.Hata hivyo Dc  alisisitiza kuwa amewasamehe baada ya kuomba msamaha.

Hatua hiyo imeibua hisia tofauti kwa wadau wa habari na haki za kiraia, huku baadhi wakieleza kuwa ni muhimu kwa vyombo vya habari kutekeleza wajibu wao wa kuhabarisha umma, hususan katika masuala yanayohusu usalama wa wananchi.

Wakati huo huo, jitihada za kupata taarifa zaidi kutoka Jeshi la Polisi mkoani humo zinaendelea ili kufahamu hatua za kisheria zinazofuata dhidi ya waandishi hao.

Tukio hili linaibua mjadala mpana kuhusu mipaka ya uhuru wa vyombo vya habari na wajibu wa mamlaka za serikali katika kutoa taarifa kwa umma, hasa katika nyakati za tahadhari ya majanga.

Post a Comment

0 Comments