MEYA ARUSHA AUNGURUMA KUHUSU MAFURIKO, ATANGAZA MABILIONI KUBORESHA BARABARA,AONYA MATUMIZI YA NGUVU KUFUNGIA MADUKA WAFANYABIASHARA

 MEYA ARUSHA AUNGURUMA KUHUSU MAFURIKO, ATANGAZA MABILIONI KUBORESHA BARABARA

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MSTAHIKI Meya wa Jiji la Arusha, Maxmilian Iranghe, amesema mvua kubwa za masika zinazoendelea kunyesha jijini humo zimeleta changamoto kubwa ya miundombinu, hasa katika kata za pembezoni ambazo zimeathirika vibaya na mafuriko.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mapema leo Marchi 27,2026, Iranghe alitaja baadhi ya kata zilizoathirika kuwa ni pamoja na Olasiti, Muriet, Terat, Moshono, Moivaro, pamoja na maeneo mengine ya pembezoni mwa jiji, ambapo barabara zimeharibika na mawasiliano kukatika.



Alisema hali hiyo imesababisha wananchi wengi kushindwa kufika katika shughuli zao za kila siku kutokana na ubovu wa barabara na kukosekana kwa njia mbadala za uhakika.

Kutokana na changamoto hiyo, Iranghe alibainisha kuwa Halmashauri ya Jiji la Arusha tayari imetenga kiasi cha shilingi bilioni tatu katika bajeti ya mwisho wa mwaka wa fedha uliopita kwa ajili ya kushughulikia ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua na vivuko, ili kupunguza athari za mafuriko.

“Mara nyingi barabara zetu hukatika kwa sababu ya kukosekana kwa mifumo imara ya kupitisha maji ya mvua. Sasa tumeelekeza nguvu kubwa katika ujenzi wa mitaro na vivuko ili kuhakikisha maji yanapita bila kuharibu barabara,” alisema Iranghe.

Aidha, aliongeza kuwa katika bajeti mpya inayoanza mwezi Julai, jiji limetenga zaidi ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya uboreshaji wa barabara katika kata zote 25 na mitaa 154, hatua inayolenga kumaliza kabisa changamoto ya miundombinu.

Alisema utekelezaji wa miradi hiyo utafanywa kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), huku sehemu ya fedha hizo ikielekezwa pia katika kuboresha barabara za eneo la kati la jiji (CBD) pamoja na kuweka taa za barabarani ili kuongeza usalama.

Iranghe alisisitiza kuwa Arusha kama jiji la utalii linahitaji miundombinu bora itakayorahisisha shughuli za kiuchumi na kuvutia wawekezaji pamoja na watalii.

Hata hivyo, aliwataka wananchi kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali za mitaa, wakiwemo madiwani na watendaji, ili kurahisisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika hatua nyingine, Meya huyo alitoa rai kwa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa sheria kutumia busara katika utekelezaji wa majukumu yao, akionya dhidi ya matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayoweza kuathiri wafanyabiashara wadogo.

Alieleza kuwa kufungwa kwa biashara bila kuzingatia mazingira kunaweza kusababisha hasara kubwa, hasa kwa wafanyabiashara wa bidhaa zinazoharibika haraka kama vyakula na mazao ya mifugo.

“Ni muhimu kutumia njia rafiki na shirikishi katika kutekeleza sheria ili kulinda uchumi wa wananchi huku tukidumisha utaratibu wa jiji letu,” alisisitiza Iranghe.

ENDS..

Post a Comment

0 Comments