MAANDALIZI MKUTANO WA TASOA ARUSHA YAPAMBA MOTO,WAJUMBE ZAIDI YA 200 NCHINI WAANZA KUMIMINIKA KAMA MVUA ARUSHA

 Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Michezo Tanzania (TASOA), Kepha Elias, amewasili jijini Arusha na kufunguka kuwa maandalizi ya mkutano mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Machi 30, 2026 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC) Arusha, yamekamilika kwa kiwango cha kuridhisha huku ukitarajiwa kuwa na uzito mkubwa kitaifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 27,2026 jijini hapa,mara baada ya kuwasili Arusha, Elias alisema mkutano huo wa kwanza wa mwaka, utakuwa wa kipekee kwa kuwakutanisha maafisa michezo kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara, kwa lengo la kujadili kwa kina maendeleo ya sekta ya michezo na kuweka dira mpya ya ukuaji wake.

Alisema mkutano huo utatoa jukwaa muhimu kwa wadau wa michezo kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazowakabili na kuweka mikakati madhubuti ya kuinua kiwango cha michezo kuanzia ngazi za chini hadi Taifa.

“Tunatarajia ushiriki mkubwa wa maafisa michezo, makocha na viongozi kutoka kote nchini. Hili ni jukwaa muhimu la kujadili mustakabali wa michezo yetu,” alisema Elias.

Alibainisha kuwa ajenda kuu zitakazojadiliwa ni pamoja na ustawi wa taaluma ya maafisa michezo, uboreshaji wa miundombinu ya michezo, pamoja na mikakati ya kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo nchini.

Aidha, alisema mkutano huo utaangazia fursa zinazotokana na mashindano ya kimataifa ikiwemo AFCON, akisisitiza kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika kiuchumi na kijamii kupitia sekta ya michezo iwapo maandalizi yatafanyika kwa umakini.

“Kupitia matukio makubwa kama AFCON, tunaweza kukuza uchumi, kuboresha miundombinu na kuinua vipaji vya wanamichezo wetu,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Katibu wa TASOA, Amani Mwaipaja, ametoa wito kwa maafisa michezo kote nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo, akieleza kuwa ushiriki wao ni msingi wa kuimarisha chama na sekta ya michezo kwa ujumla.

Mwaipaja alisema mkutano huo ni hatua muhimu katika kuijenga TASOA tangu kuanzishwa kwake, ukiwa na lengo la kuwaunganisha maafisa michezo nchini na kuweka misingi imara ya uendeshaji.

“Tunawahamasisha maafisa michezo wote kushiriki kikamilifu, kwa sababu mchango wao ndio utakaokijenga na kukiimarisha chama chetu,” alisema.

Alieleza kuwa mkutano huo pia utajadili na kukamilisha masuala muhimu ya chama ikiwemo rasimu ya katiba, mifumo ya uongozi na miongozo ya uendeshaji, hatua inayotarajiwa kuipa TASOA mwelekeo rasmi na thabiti.

Kwa mujibu wa Mwaipaja, zaidi ya maafisa michezo 200 tayari wamethibitisha kushiriki mkutano huo, huku wengine wakiwa wamewasili Arusha na wengine wakiwa njiani, jambo linaloashiria mwitikio mkubwa wa wadau wa sekta hiyo.

Aidha, aliishukuru Wizara husika kwa kutoa maelekezo kwa mikoa na halmashauri, hatua iliyochangia kuongeza ushiriki wa maafisa michezo katika mkutano huo.

Mwaipaja alisisitiza kuwa mkutano huo utatoa nafasi ya kufanya tathmini ya mafanikio yaliyopatikana, kuchambua changamoto zilizopo na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya michezo nchini.

“Maafisa michezo ndio wasimamizi wakuu wa sera na miongozo ya michezo kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa, hivyo uwepo wao hapa ni muhimu kwa mwelekeo sahihi wa maendeleo ya michezo,” aliongeza.

Viongozi hao walihitimisha kwa kusisitiza kuwa umoja wa maafisa michezo ni chachu ya maendeleo ya sekta hiyo, wakieleza kuwa kupitia mkutano huo, Tanzania inalenga kuwa na mfumo mmoja imara wa kuendeleza michezo na kuhakikisha timu za Taifa zinafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Kwa ujumla, mkutano huo wa TASOA unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika sekta ya michezo nchini, huku ukitoa dira mpya ya maendeleo jumuishi na endelevu ya michezo Tanzania.






Ends.

Post a Comment

0 Comments