HUKUMU YA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU YATUPILIA MBALI KESI YA UCHAGUZI MKUU 2020

 HUKUMU YA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU YATUPILIA MBALI KESI YA UCHAGUZI MKUU 2020

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imetoa hukumu ya kihistoria leo Ijumaa, Machi 6, 2026, kwa kuitupilia mbali kesi iliyokuwa ikipinga uhalali wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020.

Mahakama hiyo yenye makao yake makuu jijini Arusha imesema kuwa madai yaliyowasilishwa na walalamikaji hayakuwa na uzito wa kisheria wala ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa misingi ya kidemokrasia katika uchaguzi huo.

Katika uamuzi wao, majaji wa mahakama hiyo ya kikanda walibainisha kuwa pamoja na kuwepo kwa malalamiko mazito yaliyotolewa na wadai, ushahidi uliowasilishwa haukuweza kuthibitisha moja kwa moja kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi au haki za kisiasa ulioweza kuathiri uhalali wa matokeo ya uchaguzi huo.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani Novemba mwaka 2020 na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, marehemu Seif Sharif Hamad maarufu kama Maalim Seif. Baada ya kifo chake mwaka 2021, shauri hilo liliendelezwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, kwa kushirikiana na wadai wengine waliokuwa wameungana katika kesi hiyo.

Walalamikaji katika shauri hilo walijumuisha wagombea wawili pamoja na wapiga kura watatu, ambao kwa pamoja waliwasilisha madai ya kuwepo kwa matumizi ya nguvu, kukiukwa kwa haki za kisiasa za raia, pamoja na kasoro mbalimbali katika mchakato wa uchaguzi.

Hata hivyo, majaji wa mahakama hiyo walieleza kuwa pamoja na madai hayo kuwa makubwa na yenye uzito katika mjadala wa kisiasa, ushahidi uliowasilishwa haukutosha kuonyesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya tuhuma hizo na ukiukwaji wa sheria au mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu inayotambuliwa na mahakama hiyo.

Aidha, walalamikaji walikuwa pia wakiiomba mahakama hiyo kutoa maelekezo kwa Serikali ya Tanzania kufanya mageuzi ya Katiba na sheria za uchaguzi ili kuimarisha zaidi mfumo wa demokrasia na haki za kisiasa nchini.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, mahakama imeeleza kuwa madai hayo hayakuweza kuthibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa kisheria, hivyo kuamua kuyatupilia mbali.

Uamuzi huo unahitimisha rasmi shauri lililovuta hisia za wadau wengi wa siasa, sheria na haki za binadamu katika ukanda wa Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla, huku ukiweka kumbukumbu muhimu katika historia ya kesi zinazohusu michakato ya kidemokrasia barani Afrika.


Ends..

Post a Comment

0 Comments