TAASISI YA TWARIQA ARUSHA YAFUTURISHA MAMIA YA WAISLAMU, YAKESHA KUMWOMBEA DUA RAIS SAMIA,SHEIKH HARUNA ALAMBA UKATIBU MKUU TAIFA,YAMUENZI MAREHEMU SALIMU DARUWESSHI

 TAASISI YA TWARIQA ARUSHA YAFUTURISHA MAMIA YA WAISLAMU, YAMUENZI MAREHEMU SALIMU DARUWESSHI

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


Taasisi ya Dini ya Kiislamu ya Twariqa, Zawia Kuu ya Arusha, imeandaa hafla kubwa ya futari iliyowakutanisha mamia ya waumini wa Kiislamu kutoka mikoa mbalimbali nchini, katika tukio lililolenga kusherehekea mwezi mtukufu wa Ramadhani pamoja na kumuenzi aliyekuwa kiongozi wa taasisi hiyo, Marehemu Salimu Daruwesshi maarufu kwa jina la Mti Mkavu.

Hafla hiyo ilifanyika katika mazingira ya ibada, mshikamano na shukrani, ambapo waumini walipata fursa ya kushiriki futari ya pamoja, kufanya dua na kuombea amani ya taifa. Katika mkesha wa dua uliofanyika wakati wa tukio hilo, waumini walimuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na taifa kwa ujumla ili kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa.


Katika hatua nyingine muhimu ya tukio hilo, Sheikh Haruna Lotta Husein alitangazwa rasmi kuwa Katibu Mkuu wa Twariqa Taifa. Akiwahutubia washiriki wa hafla hiyo, Sheikh Haruna alitoa shukrani zake kwa viongozi wa taasisi na jamii ya Kiislamu kwa kumuamini na kumpa jukumu hilo kubwa.

Sheikh Haruna, ambaye hapo awali alikuwa akihudumu kama Naibu Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, alisema kuwa nafasi hiyo ni dhamana nzito inayohitaji ushirikiano wa pamoja ili kuhakikisha miradi na mipango ya maendeleo ya taasisi inatekelezwa kwa ufanisi.

“Ni heshima kubwa na jukumu la kipekee kupokea nafasi hii. Ninaahidi kufungua milango ya kushauriana na kushirikiana na waislamu wote ili kuhakikisha taasisi yetu inatekeleza malengo yake kwa manufaa ya jamii nzima,” alisema Sheikh Haruna.


Aliongeza kuwa katika kipindi chake cha uongozi atahakikisha taasisi hiyo inaweka mikakati ya kubuni na kuendeleza miradi endelevu itakayoiwezesha kujitegemea kiuchumi, badala ya kutegemea msaada kutoka kwa wahisani pekee.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa waislamu, huku akitoa shukrani kwa serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuongoza taifa kwa hekima na busara chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika tukio hilo pia kulifanyika utangazaji rasmi wa viongozi mbalimbali wa kada tofauti ndani ya taasisi hiyo, hatua inayolenga kuimarisha mfumo wa uongozi na kuongeza uwazi katika usimamizi wa shughuli na miradi ya Twariqa Taifa.


Awali, kiongozi wa taasisi hiyo kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, Sheikh Halfa Jafar Fundi Haji, alitangaza rasmi viongozi wapya wa taasisi hiyo na kuwataka kufanya kazi kwa umoja, uadilifu na kujituma kwa lengo la kuendeleza maendeleo ya taasisi pamoja na jamii kwa ujumla.

Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha viongozi na wanachama wa taasisi hiyo, Sheikh Halfa Jafar alisema uteuzi wa viongozi hao ni sehemu ya kuimarisha uongozi na kusukuma mbele malengo ya taasisi hiyo ya kiroho na kijamii.

Alieleza kuwa viongozi walioteuliwa kuanzia ngazi ya Naibu Sheikh hadi Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu wanapaswa kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha taasisi inaendeshwa kwa misingi ya uwazi, mshikamano na uwajibikaji.

“Tunawashukuru sana viongozi wote waliokubali dhamana hii. Tunaamini wataitumikia taasisi kwa moyo wa kujitolea na kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa mafanikio,” alisema Sheikh Halfa Jafar.

Aidha, aliwashukuru wanachama wa makundi mbalimbali ambao wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiimani za taasisi hiyo, ikiwemo harambee na mipango mingine ya maendeleo inayolenga kuimarisha ustawi wa taasisi na jamii.

Alibainisha kuwa ushirikiano uliopo miongoni mwa wanachama umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa taasisi hiyo na kuongeza mshikamano ndani ya jamii ya waumini.

Katika mkutano huo, washiriki pia walipata fursa ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya taasisi na kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano ili kuendeleza shughuli zake katika siku zijazo.

Sheikh Halfa Jafar Fundi Haji alisisitiza kuwa viongozi wapya wanapaswa kuweka mbele maslahi ya taasisi na kuhakikisha wanadumisha umoja, amani na ushirikiano miongoni mwa wanachama.

Mwisho, alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha kufanyika kwa mkutano huo na kuwataka waumini kuendelea kushikamana ili kuimarisha taasisi pamoja na kuleta maendeleo katika jamii. Pia alitoa shukrani kwa waandishi wa habari kwa kujitokeza na kuripoti tukio hilo.

Tukio hilo limeendelea kuwa kielelezo cha mshikamano wa waumini wa Kiislamu, uwazi katika uongozi wa taasisi za dini, pamoja na matarajio mapya ya maendeleo endelevu na kujitegemea kwa Twariqa Taifa.










Mwisho.

Post a Comment

0 Comments