ASKOFU MONABAN AINGIZWA RASMI KKAM, AAHIDI KUWATETEA WANYONGE
Hatua yatajwa kuwa alama ya uongozi mpya wa kiroho na kijamii Kanda ya Kaskazini
Na Joseph Ngilisho | Arusha
ASKOFU Dk. Philemon Mollel “Monaban” amewekwa rasmi kazini kuwa Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM) katika ibada maalum iliyofanyika Parokia ya Ngulelo jijini Arusha, tukio lililotajwa na viongozi wa dini kuwa mwanzo wa enzi mpya ya uongozi unaolenga haki, huduma jumuishi na utetezi wa wanyonge katika jamii.
Ibada hiyo ya kihistoria ilihudhuriwa na mamia ya waumini, maaskofu na wachungaji, pamoja na viongozi wa serikali na wageni waalikwa kutoka zaidi ya mikoa 21 nchini. Waumini walijaa kanisani kwa shangwe, wakimpongeza kiongozi huyo kwa zawadi na sala za baraka, wakionesha imani kubwa kwa uongozi wake.
Katika kilele cha ibada, Askofu Mollel aliweka nadhiri ya utumishi akiahidi kuongoza kwa haki, upendo na bila ubaguzi, huku akisisitiza dhamira yake ya kusimama na wanyonge.
“Naahidi mbele za Mungu na waumini kuwatumikia kwa uaminifu na bila ubaguzi. Nitasimama kwa ajili ya walio dhaifu na kuhubiri kweli bila woga,” alisema.
Baada ya nadhiri hiyo, viongozi wa kanisa walimbariki rasmi na kumkabidhi majukumu ya kichungaji katika nafasi hiyo ya juu ya uongozi.
Akiongoza ibada hiyo, Askofu Mkuu wa KKAM, Askofu Mkuu Oscar Olutu, aliwataka viongozi wa dini kusimama imara katika kweli na kuhubiri bila hofu, akisisitiza kuwa uongozi wa kiroho unahitaji ujasiri, unyenyekevu na uwajibikaji kwa jamii.
Akizungumzia historia ya kanisa, Askofu Olutu alibainisha kuwa KKAM lililoanzishwa mwaka 1999 sasa lina zaidi ya parokia 136, wachungaji na mashemasi zaidi ya 160 pamoja na dayosisi nane — hatua inayoakisi kupanuka kwa kasi kwa huduma za kiroho nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi Ahmed Mwinyi, Afisa Tarafa wa Moshono, Dominick Njunwa, alisema serikali imepokea maombi ya kanisa na itayafanyia kazi kwa mujibu wa taratibu.
Kuingizwa rasmi kwa Askofu Mollel kunatazamwa kama mwanzo wa sura mpya ya uongozi ndani ya KKAM, huku waumini wakionesha matumaini makubwa kwa mchango wake katika huduma za kiroho na ustawi wa jamii kanda ya kaskazini.
Ends.





0 Comments