MGONJWA AFARIKI BAADA YA AMBULANCE KUPATA AJALI NJIANI KWENDA HOSPITALI TANGA
By Arushadigital – Tanga
Mgonjwa mmoja amefariki dunia huku watu wanne wakijeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha gari la wagonjwa (ambulance) na lori kugongana uso kwa uso katika eneo la Saruji, kando ya barabara kuu ya Tanga–Segera.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Tanzania, ajali hiyo ilitokea Machi 1, 2026 majira ya saa 6:10 usiku. Ililihusisha gari la wagonjwa aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili STM 7202, mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, lililokuwa likitokea Mombo kuelekea Tanga Mjini.
Ambulance hiyo iligongana na lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 628 DSG likiwa na tela namba T 637 DSG, lililokuwa likitokea Tanga kuelekea Arusha.
Marehemu ametambuliwa kuwa Zaharia Abrahaman Mdoe (41), mkazi wa Goha wilayani Korogwe, ambaye alikuwa akisafirishwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bombo kwa ajili ya matibabu zaidi.
Waliopata majeraha katika ajali hiyo ni Zainabu Abrahaman Mdoe, Seleman Hassan Mdoe, Naiman Msofe Mdoe pamoja na muuguzi Hatibu Deusi Hatibu, wote waliokuwa ndani ya gari hilo la wagonjwa wakati wa tukio.
Taarifa za awali za polisi zinaeleza kuwa chanzo cha ajali kinahusishwa na mwendokasi wa dereva wa ambulance, hali iliyosababisha kushindwa kulimudu gari na kupelekea kugongana na lori hilo.
Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Ends.




0 Comments