WAZIRI WA UJENZI AKAGUA DARAJA LA KING’ORI ARUMERU, ATOA ONYO KWA WAKANDARASI WAZEMBE
Miradi 81 ya miundombinu yenye thamani ya Sh bilioni 500 yatekelezwa; taa 136 kuwekwa barabara ya KIA–Arusha
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi imetekeleza jumla ya miradi 81 ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara yenye thamani ya shilingi bilioni 500, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100 za uongozi wake katika sekta ya miundombinu.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Daraja la King’ori katika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Waziri wa Ujenzi, Dkt. Abdallah Ulega, amesema kati ya miradi hiyo, 40 imekamilika kwa asilimia 100, ikiwemo mradi wa daraja hilo muhimu linalorahisisha usafiri na uchumi wa ukanda huo.
Ameeleza kuwa mradi huo pia unahusisha uwekaji wa taa 136 za barabarani kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) hadi Jiji la Arusha, hatua inayolenga kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara, hususan nyakati za usiku, na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi na watalii.
Katika hatua nyingine, Dkt. Ulega ametoa onyo kali kwa wakandarasi na wasimamizi wa miradi wanaochelewesha utekelezaji wa miradi ya barabara nchini, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria endapo uzembe utabainika.
Amesema wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kupitia mikataba ya baadhi ya wakandarasi wa nje wanaokwamisha miradi, na kubainisha vipengele vinavyokiukwa kisheria ili hatua stahiki zichukuliwe.
“Hatutasita kuvunja mikataba ya wakandarasi wazembe. Mfano ni Mkoa wa Kagera ambako shilingi bilioni 9 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara lakini utekelezaji wake hauridhishi,” amesema Waziri Ulega.
Aidha, Waziri huyo ametangaza mwelekeo mpya wa Serikali katika utoaji wa zabuni, akieleza kuwa miradi yote yenye thamani isiyozidi shilingi bilioni 50 itatekelezwa na wakandarasi wazawa ili kukuza uwezo wa ndani. Miradi mikubwa zaidi itatekelezwa kwa ushirikiano kati ya wakandarasi wa nje na wazawa kwa lengo la uhamishaji wa ujuzi na teknolojia.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msondo, amesema mafanikio ya miradi hiyo ndani ya siku 100 yanaashiria dhamira ya Serikali ya kuimarisha miundombinu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mwinyi, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makalla, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika mkoa huo, akieleza kuwa miradi hiyo imeanza kuleta matokeo chanya kwa wananchi na shughuli za kiuchumi.
Ends









0 Comments